Basi la abiria kutoka mkoani Dodoma, Safari Njema na lori lenye tela lililokuwa limebeba mifuko ya saruji, yameteketea kwa moto na kusababisha kifo cha mtu na msongamano wa magari kwenye Barabara Kuu ya Dar – Morogoro. Magari hayo yameungua baada ya kugongana jana mchana.
Ajali hiyo ilitokea saa nane mchana.baada ya lori kupoteza mwelekeo na kuligonga basi ambalo lilijaribu kulikwepa, lakini likagongwa ubavuni na kusababisha mlipuko na kuwaka moto magari yote mawili.
Basi hilo lina namba za usajili T 990 AQF wakati lori liliteketea kabisa kichwa chake, lakini tela lake lenye namba za usajili T 534 BYJ limebaki.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Garage, Kimara kati ya Suka na Stop Over wilaya mpya ya Ubungo katika Barabara Kuu ya Dar – Morogoro, na kusababisha kifo cha mtu mmoja ambaye ameungua moto kiasi cha kutotambulika.
Watoto watano na wadada wanne wameripotiwa kuokolewa dakika 15 baada ya magari hayo kuwaka moto, huku abiria wengine wa basi hilo wakiruka kwa nia ya kuokoa maisha yao katika ajali hiyo mbaya.
Hadi jana saa 12.30 jioni, bado magari hayo yalikuwa eneo la ajali na kulikuwa na msururu mrefu wa magari kutoka eneo la Mbezi kwenda jijini Dar es Salaam pamoja na kutoka jijini Dar es Salaam kwenda nje ya Jiji na mikoani na abiria walikuwa wakitembea kwa miguu.
Wakati huo askari wa trafiki ndio walifika eneo la tukio.
Akizungumza katika eneo la ajali jana saa 12.45 jioni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Suzan Kaganda alithibitisha kifo cha mtu mmoja ambaye anaelezwa kuwa ni mtoto, na amehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa utambuzi zaidi.
Kamanda Kaganda alieleza kuwa ajali hiyo imesababisha majeruhi 16 ambao kati yao, 10 hali zao ni mbaya na wamelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakati sita waliruhusiwa kurejea makwao baada ya kutibiwa kwani walipata mshtuko tu..