Wiliam Ngeleja arejesha fedha za mgao wa ESCROW alizopokea Disemba 2, 2014.
Wiki kadhaa baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumpandisha kizimbani mfanyabiashara James Rugemalira, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja amerudisha fedha alizopokea kutoka kwa mfanyabiashara huyo miaka mitatu iliyopita.
Ngeleja amezungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Julai 10, na kueleza kuwa fedha hizo zipatazo Sh 40.4 milioni tayari ameshazikabidhi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Fedha hizo ni sehemu ya Sh 306 bilioni zilizochotwa kwenye akauti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kwa pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni ya kufua umeme ya IPTL wakati wakisubiri mzozo wa kimkataba baina yao uliokuwa mahakamani umalizike.
Fedha hizo ziligawiwa kwa wanasiasa akiwamo Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, majaji, wabunge na viongozi wa dini.
Ngeleja amesema ameamua kuzirudisha fedha hizo baada ya Rugemalira kuhusishwa na kashfa ya akaunti hiyo ya Escrow.
"Nilipokea msaada huo kama wapokeavyo wabunge wengine, ilikuwa ni msaada ambao nilipewa kwa ajili ya jimbo langu bila kujua kwamba Rugemalira baadaye angekuja kuhusishwa na kashfa ya fedha, za akaunti ya Escrow."
"Nimepima na kutafakari na hatimaye nimeamua kwa hiari yangu kurejesha serikalini fedha zote nilizopewa kama msaada bila kujali nilishazilipia kodi ya mapato," amesema.
Amesema ameamua kurudisha fedha hizo hata kama aliyempa msaada bado ni mtuhumiwa.
"Ninarudisha fedha hizi ili kulinda heshima na maslahi mapana ya nchi, chama, Serikali, jimbo langu la Sengerema, familia yangu na heshima yangu mwenyewe,"amesema.
===>
No comments:
Post a Comment