Wambura analipwa Mil.7.....Kasema watia saini TFF walighushiwa
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura (49) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anapokea mshahara wa Shilingi Milioni 7 kwa mwezi.
Wambura ameyaeleza hayo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili, aiyekuwa rais wa TFF Jamal Malinzi na wenzake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Akiongozwa na wakili wa utetezi, Richard Rweyongeza kutoa ushahidi wake, Wambura amebainisha kuwa aliwahi kuwasilisha maombi ya kutaka kuongezwa mshahara kutoka Shilingi Milioni 2 hadi 7 wakati wa utawala wa Malinzi.
Alipoulizwa na wakili Rweyongeza kwamba Malinzi alikataa kumuongeza mshahara, Wambura alidai kuwa si kweli, lakini alipeleka maombi hayo tena wakati wa utawala wa Rais wa sasa wa TFF, Walles Karia ambapo ameidhinisha alipwe Shilingi Milioni 7 tangu August 2017 hadi sasa.
Awali akiongozwa na Wakili wa serikali, Shadrack Kimaro, Wambura alidai kuwa muhtasari wa June 5,2016 uliokuwa na ajenda ya kubadilisha watia saini wa akaunti za Benki za TFF zilizopo Stanbic ni wa kughushi na kwamba yeye haufahamu.
Wambura amedai anasema hayo kwa sababu alikuwepo katika kikao hicho cha June 5,2016 na hakukuwepo na ajenda ya kubadilisha watia saini wa benki wa TFF kwa kumtoa Edgar Masoud na kumuingiza Nsiande Mwanga.
Baada ya kueleza hayo, kesi hiyo imeahirishwa hadi May 28 na 29 , 2018 kwa ajili ya kuendelea kusikiliza kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Katika kesi hiyo washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine, Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga. Pia Meneja wa Ofisi wa (TFF),Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya.
Kwa pamoja washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 30 ikiwemo kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa USD 173,335 na Sh 43,100,000.
No comments:
Post a Comment