Nyalandu akabidhiwa kadi ya Chadema
Nyalandu aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini kwa tiketi ya CCM alijiondoa ndani ya chama hicho Oktoba 30,2017.
Kadi ya Chadema amekabidhiwa jana Jumapili Novemba 19,2017 katika uwanja wa Shule ya Msingi Mhandu ambako Mbowe alihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za udiwani katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 26,2017.
"Nimeisubiri kwa shauku kubwa siku hii ya leo ili nipate fursa ya kupigania mageuzi ya kisiasa na ya kiuchumi Tanzania," alisema Nyalandu baada ya kukabidhiwa kadi.
Alisema ana shauku, furaha na heshima kukaribishwa rasmi kuwa mwanachama wa Chadema.
Nyalandu alisema katika majira na nyakati ambazo Taifa linapitia, mabadiliko ya kisiasa nchini Tanzania ni lazima.
"Naungana na chama hiki pendwa ili tutembee pamoja mtaa kwa mtaa kijiji kwa kijiji tuwaambie wananchi wakati wa ukombozi ni sasa," alisema Nyalandu.
Amesema haki huinua Taifa, hivyo wakiungana litainuka.
"Saa ya mabadiliko imefika kwa mtu yeyote miongoni mwetu, tumepewa utayari wa kubadilisha mwelekeo wa nchi," alisema.
Mbowe alimnadi Godfrey Misana anayewania udiwani katika Kata ya Mhandu pasipo yeye kuwepo kutokana na kuwa mahabusu alikopelekwa kwa kukabiliwa na shtaka la kujeruhi.
No comments:
Post a Comment