Tume
ya vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesema kuwa kesho Agosti 15, 2018 ndiyo
mwisho wa kutuma maombi ya kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza
katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini.
Dirisha hilo la kuwasilisha maombi lilifunguliwa Julai 20, 2018 kwa awamu ya kwanza.
Akizungumza
leo Agosti 14, 2018 Katibu Mtendaji wa TCU Profesa Charles Kihampa
amesema kuwa baada ya kufungwa rasmi kwa dirisha la udahili vyuo
vitaanza kuchakata majina ya waombaji kulingana na vigezo vya udahili
vilivyowekwa kwa kila programu ya masomo.
Udahili
wa kujiunga na vyuo vikuu unahusu makundi makubwa matatu ambayo ni
waombaji wa kidato cha sita, wenye sifa linganifu kama vile shahada na
waombaji wenye vyeti toka nje ya nchi vyenye sifa linganifu.
"Baada ya kuchakata majina, dirisha la waombaji litaidhinishwa, " amesema Kihampa na kuongeza:
"TCU
jukumu lao ni kuhakiki kama waombaji waliochaguliwa na vyuo wana sifa
stahiki na wanakidhi vigezo vya kujiunga na programu husika za
masomo,"amesema Profesa Kihampa.
Amefafanua
kuwa waombaji wote wa udahili wanapaswa kutuma maombi yao moja kwa moja
kwenye vyuo wanavyopenda na kuchagua programu za masomo.
Amesema
Tume imetoa mwongozo wa programu zilizoidhinishwa kudahili pamoja na
vigezo vya udahili vinavyotakiwa kwa kila programu za masomo.
"Waombaji
wote wa vyuo vikuu na taasisi ya elimu ya juu wanakumbushwa na
kuhimizwa kuzingatia kalenda ya udahili iliyoidhinishwa na Tume,"amesema
Kihampa na kuongeza:
"Ili kuepusha usumbufu usio wa lazima, waombaji wote wanahimizwa kutumia muda uliobaki kukamilisha maombi yao.”
No comments:
Post a Comment