Mtuhumiwa Aliyetoroka akiwa chini ya ulinzi atupwa jela mwaka mmoja
Mahakama ya Mwanzo Kinondoni, imemhukumu Allen Robert (33) kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la kutoroka akiwa chini ya ulinzi mahakamani.
Mtuhumiwa huyo anayekabiliwa na kesi ya kujaribu kubaka alitoroka akiwa chini ya ulinzi wa askari magereza mara baada ya kutoka kusikiliza ushahidi wa kesi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Marko Mochiwa baada ya askari magereza mwenye namba B.4296 Koplo John Chale kutoa maelezo ya jinsi Robert alivyotoroka na kukimbia.
Hakimu Mochiwa ametoa hukumu hiyo baada ya kupitia maelezo ya mlalamikaji ambapo amesema kitendo cha kukimbia akiwa chini ya ulinzi ni kinyume kwa mujibu wa sheria za Jamhuri.
Katika utetezi wake mtuhumiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ana kesi nyingine inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Awali mwendesha mashtaka wa polisi alimsomea hati ya mashtaka mtuhumiwa huyo na kudai kuwa wakati alipokuwa akitoka nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni baada ya kutoka kwenye kesi ya kubaka akielekea katika chumba cha mahabusu ghafla alitoroka na kukimbia.
No comments:
Post a Comment