Polisi Watumia Risasi Kumkamata Mtuhumiwa Aliyetoroka Chini ya Ulinzi wa Askari Magereza
Mshtakiwa anayekabiliwa na kesi ya kujaribu kubaka Allen Robert (33), ametoroka akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza baada ya kutoka kusikiliza ushahidi wa kesi inayomkabili na kusababisha taharuki kwa baadhi ya wananchi waliokuwa eneo hilo.
Tukio hilo lilitokea jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni jijini Dar saa tisa alasiri na askari Magereza walilazimika kurusha risasi hewani ili kumkamata.
Wananchi waliohudhuria mahakamani kwa shughuli mbalimbali baadhi walikimbia baada ya kusikia milio ya risasi.
Mmoja wa wananchi waliokuwa eneo hilo, Alex Simon alisema baada ya kusikia milio ya risasi aliingia chini ya meza na alilala chini akihofia usalama wake.
“Wakati nikiwa nimeagiza chakula kwenye mgahawa ghafla niliona mtu akitoka hapo kwenye geti la Mahakama kisha nikasikia sauti ya askari Magereza wakisema lala chini wakati huo yule mshtakiwa akikimbia katikati ya watu. Nililala chini ya meza baada ya dakika 15 hali ilikuwa shwari,” alisema Simon.
Baada ya Robert kukamatwa alifunguliwa shtaka na kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni kwa kutoroka akiwa chini ya ulinzi.
Mbele ya Hakimu Marko Mochiwa, Mwendesha mashtaka wa Polisi, Mrusha Warioba alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 10 katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni.
“Mshtakiwa unakabiliwa na shtaka la kumtoroka askari Magereza Koplo John Chale, ulifanya hivyo ukijua kwamba ni kinyume na sheria,” alidai Warioba.
Baada ya maelezo hayo mshtakiwa hakujibu chochote licha ya kuulizwa zaidi ya mara mbili.
Hakimu Mochiwa aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 16 kesi hiyo itakaposikiliza. Mshtakiwa alipelekwa rumande.
Katika kesi ya msingi iliyopo mbele ya Hakimu Issa Kasailo, mshtakiwa anakabiliwa na shtaka la kujaribu kumbaka binti mwenye umri wa miaka 24.
Kesi hiyo ilitajwa mahakamani hapo jana kwa ajili ya kuendelea na ushahidi na shauri liliahirishwa hadi Mei 24.
No comments:
Post a Comment