TRA Yazifunga Ofisi za Yusuf Manji
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezifunga ofisi za kampuni ya mfanyabiashara Yusufu Manji kutokana na kudaiwa Sh 12.2 bilioni.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo amesema wamekuwa na mawasiliano na kampuni ya Farm Equpment ambayo inamilikiwa na Manji tangu Agosti 15 mwaka huu lakini kulikuwa hakuna mrejesho kuhusu deni hilo.
Kutokana na hilo amesema wamefunga ofisi zake kwa sababu kampuni hiyo inadaiwa kiasi cha Sh 12.2 bilioni lakini kampuni hiyo ina nafasi ya kuendelea kuwasiliana na TRA namna ya kulipa deni hilo.
Tukio hilo limetokea leo Jumatatu kati ya saa 4 hadi 7 wakati TRA na kampuni ya udalali ya Yono wakiambatana na polisi walipokwenda katika jengo hilo lililopo barabara ya Pugu, wilayani Temeke.
Baadhi ya mashuhuda wakiwamo walinzi kwa masharti ya kutotaja majina yao wamesema kuwa ofisi zilizofungwa ni ya Manji na sehemu yake duka la kuuza pikipiki na matrekta.
Wamesema baada ya kufika watu waliingia moja kwa moja katika ofisi yake kisha kufanya majadiliano na wahusika yaliyodumu zaidi ya saa 2.
"Nadhani hawakufikiana mwafaka kwa sababu walivyotoka wakaamuru wafanyakazi wa ofisi hiyo kutoka nje kisha kuweka utepe wa rangi nyekundu na nyeupe," amesema shuhuda huyo.
Hata hivyo, mashuhuda hao wamesema hawajui tatizo ni nini lakini waliwasikia maofisa wa TRA na kampuni hiyo ya udalali wakizungumza kuhusu kodi.
No comments:
Post a Comment