Watu Wanne Wahukumiwa Kwenda Jela Miaka 30 Na Viboko 12.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu watu wa nne kutumikia kifungo cha mika 30 jela na kuchapwa viboko 12, sita wakati wa kuingia na sita wakati wa kutoka baada ya kupatikana na hatia dhidi ya kosa la wizi wa kutumia silaha.
Hukumu hiyo iliyosomwa na hakimu Mkazi, Respicious Mwijage imewataja waliofungwa kuwa ni Donald Nzweka, Michael Pascal,Ally Akili na Kurwa Mwakagenda.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mwijage alisema, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka na kuwa washtakiwa walishiriki kutenda kosa na kwamba mahakama ilijiuliza kwamba kosa la kutumia silaha ili lithibitike Jamhuri wana wajibu wa kuthibitisha bila kuacha shaka kwamba mshtakiwa kabla ya kutenda awe na kifaa hatari au wawe zaidi ya mmoja na kwamba baada ya tukio hilo walitumia nguvu kwa mtu waliyepora.
Katika kesi hii, mlalamikaji na mashahidi wengine walieleza kuwa usiku wa julai 7 majambazi walivunja mlango mkuu wa nyumba yao kwa kutumia bomu ambalo lilitambuliwa na polisi kuwa baruti na kisha kuendelea kuvunja milango mingine ambapo baada ya hapo waliingia katika chumba walichokuwa wamekaa, ambacho kilikuwa na mwanga, mshtakiwa mmoja alishika panga na kuanza kuwapiga kwa kutumia ubapa.
Alisema, kwa kuzingatia ushahidi huo hakuna shaka kwamba mashahidi waliweza kuwatambua majambazi na kuwa utetezi wa washtakiwa kwamba walikamatwa maeneo tofauti na kupelekwa oysterbay polisi na kupigwa na kunyanyaswa siyo ya kweli.
Kabla ya kusomwa kwa adhabu hiyo, Hakimu Mwijage aliuliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote na kusema juu ya washtakiwa ambapo wakili wa serikali Gloria Mwenda, alidai washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na akaomba wapewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa jamii.
“Nimeridhika ushahidi wa mashahidi 11 walioletwa na upande wa mashtaka ambao wameweza kuthibitisha bila ya kuacha shaka kuwa mlitenda kosa, nawahukumu kwenda jela miaka 30 na kuchapwa viboko 12, sita siku mnaingia na sita siku ya kutoka" alisema Mwijage.
Awali ilidaiwa, Julai 7 ,2013 huko maeneo ya Boko Magengeni, jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao waliiba simu nne pesa taslimu 150,000 na cheni za dhababu mbili ambapo vitu vyote vina thamani ya 2, 050,000 mali ya Hobokela Mwakijambile.
No comments:
Post a Comment