Waziri Kairuki Aelezea Vipaumbele Vyake Wizara ya Madini
Kairuki ameyasema hayo jana tarehe 10 Oktoba, 2017 jijini Dar es Salaam alipozungumza na watumishi wa Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake, waliopo Dar es Salaam na Makao Makuu ya Wizara Dodoma.
Lengo La kikao hicho lilikuwa ni kufahamiana na kupanga mikakati ya kushirikiana ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa Uchumi wa nchi.
Taasisi zilizoshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma (MRI) pamoja na Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini na Mpango wa Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (TEITI).
Alisema kuwa Sekta ya Madini inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwataka wataalam wa madini kubuni mbinu za ukusanyaji wa maduhuli pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye uchimbaji madini.
Katika hatua nyingine aliwataka wataalam hao kubuni mikakati ya kuzuia utoroshaji wa madini nchini ili nchi ipate mapato stahiki.
Aliwataka watumishi kuepuka kufanya kazi kwa mazoea na kuwa wabunifu ili sekta hiyo iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Naye Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliwakumbusha watumishi kuzingatia Dira na Dhima ya Wizara ikiwemo kufanya kazi kwa tija ili hatimaye sekta ya madini iweze kuchangia katika uchumi wa nchi kwa kuwa mchango wa sekta husika bado ni kidogo.
No comments:
Post a Comment