Mawakili kesi ya Kitilya na wenzake walalamikia upelelezi......Wataka Kesi Ifutwe
Upande wa utetezi umeiomba Mahakama kuulazimisha upande wa mashtaka kuifuta kesi ya utakatishaji fedha, inayomkabili aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya na wenzake.
Wakili wa utetezi, Majura Magafu ametoa ombi hilo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mbele ya Hakimu Mfawidhi Cyprian Mkeha wakati kesii hiyo ilipokuja kwa kutajwa.
Aliiomba mahakama kuwa, upande wa mashtaka ulazimishwe kesi ifutwe ama waiondoe mahakamani kwa sababu washtakiwa awali walikuwa chini ya dhamana na wakiripoti kila walipohitajika Takukuru.
Wakili wa utetezi, Majula Magafu alidai kuwa sasa imefikia wakati mahakama ihakikishe maelekezo inayoyatoa yanaheshimiwa
"Mahakama inaweza kuifuta kesi ili ushahidi ukikamilika waletwe tena, kwa sababu imebaki hadithi kila wakija wanasema wanasubiri vielelezo kutoka Ulaya na miaka inaenda tu,".
Akijibu hayo, wakili wa serikali, Constantine Kakula alidai upelelezi wa kesi hiyo unashindwa kukamilika kwa sababu inahusisha uchunguzi unaovuka mipaka.
Alidai, siyo kama jamhuri imelala bali inafanya mawasiliano na upande wa pili, kwa sababu hatuwezi kumlazimisha anayetuma nyaraka za upelelezi kutoka Ulaya.
Hakimu Mkeha akautaka upande wa mashtaka kuhakikisha unakamilisha upelelezi.
Kitilya na wenzake, aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na Sioi Solomon wanashtakiwa kwa utakatishaji wa fedha dola milioni 6. Kesi hiyo imeahirishwa hadi September 8/2017.
No comments:
Post a Comment