Kikwete aitamani nafasi ya Kinana CCM
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amesema hatamani kuwa rais bali anataka siku moja awe Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam juzi alipohojiwa katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na Televisheni ya Clouds.
Jibu hilo la Ridhiwani lilitokana na swali aliloulizwa na watangazaji wa kipindi hicho kama ana ndoto za kuwa rais wa nchi.
“Sijawahi kutamani kuwa rais ila muda ukifika natamani kuwa Katibu Mkuu wa CCM,” alisema.
Ridhiwani alisema mafaniko yake hadi hapo alipofikia ni kutokana na mchango wa baba yake ambaye ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
“Malezi yangu, kuzaliwa na kiongozi kumenisaidia kufika hapa, nisingezaliwa huko labda ningekuwa mtu tofauti na nilivyo, mzee wangu ana mchango mkubwa hata jimboni, ananipa changamoto, ananielekeza, ana nafasi ya kunishauri,” alisema.
Pia alisema katika kutekeleza sera ya Tanzania ya viwanda, tayari Mkoa wa Pwani una viwanda 164 vikiwamo vinavyojengwa na vilivyokamilika, huku 84 vikiwa ni vikubwa.
Alisema uwekezaji wa viwanda hivyo umegawanyika katika sehemu mbili, chini ya Sh bilioni tano na ule ulio juu zaidi.
“Sehemu kubwa ni viwanda vya kuchakata malighafi, kuna vya matunda, marumaru, nondo, korosho, mabati, saruji na malighafi ya nyumba na vinavyofanya kazi nikivitaja ni zaidi ya 40,” alisema.
Ridhiwani alisema jimbo lake na mkoa wote wa Pwani, unafanya jitihada kuhakikisha bidhaa zilizokuwa zikipatikana China ziweze kupatikana Chalinze ili kuepuka gharama za usafirishaji.
Alisema uwekezaji wa kiwanda cha Twyford Tanzania Ceramics kilichotembelewa wiki hii na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, uligharimu Dola za Marekani milioni 158.
Ridhiwani alisema kiwanda hicho kinachotarajia kukamilika katika kipindi cha Julai hadi Agosti, kitakuwa na uwezo wa kutoa kontena 28 hadi 30 kwa siku.
Alisema kupitia kiwanda hicho, wananchi watapata faida kwa kufanya biashara na kuongezeka kwa ajira.
“Kitakuwa na ajira zaidi ya 2,000 zilizo rasmi, huku zisizo rasmi zikiwa ni zaidi ya 4,000. Hata hivyo, bado nasisitiza ajira izingatie wazawa kwa sababu wananchi tayari wanalalamikia upendeleo katika kupeana ajira, walioajiriwa pale wengi si wakazi wa Chalinze, hata Waziri Mwijage nilimwambia,” alisema.
Pamoja na jitihada hizo, alisema utekelezaji wa sera ya Tanzania ya viwanda unaweza ukakwamishwa kutokana na uwezo wa kutafsiri neno na nia nzuri ya Rais Dk. John Magufuli.
“Rais hawezi kujenga viwanda peke yake, wasaidizi tutoe tafsiri sahihi ya nia yake nzuri, tutekeleze. Sitokubali kumdhalilisha rais, akisimama mwaka 2020 akiulizwa kuwa viwanda viko wapi aseme viko Pwani, atoe mfano Chalinze,” alisema.
No comments:
Post a Comment