Rais Museveni Kuwasili Nchini Jumamosi
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni anatarajiwa kufanya ziara ya siku mbili nchini kuanzia Jumamosi wiki hii.
Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiao wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuendeleza uhusiano mzuri uliopo baina ya Uganda na Tanzania, pamoja na kujadili masula mbalimbali ya kikanda, kimataifa na sekta mbalimbali za ushirikiano kati ya nchi hizi mbili hususani katika sekta za nishati, biashara na uchukuzi.
“ Mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Uganda yameendelea kuimarika katika miaka ya hivi karibuni, ambapo mwaka 2016 Tanzania ilifanya mauzo nje kwa Nchi hiyo ya kiasi cha shilingi bilioni 66.849, ikilinganishwa na shilingi bilioni 78.31 za mwaka 2015” alisema Waziri Mahiga.
Aliongeza kuwa Uganda ni muhimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo haina Bandari na hivyo inategemea Tanzania kwa ajili ya kupitisha mizigo yake.
Nchi ya Uganda imezidi kuwa na umuhimu kufuatia uamuzi wa kupitisha bomba la mafuta nchini Tanzania, kutoka Kabaale –Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, ambapo bomba hilo lina urefu wa kilimeta 1443 na kipenyo cha inchi 24.Bomba hilo la mafuta litakalokamilika mwaka 2020 limnatarajiwa kupatia nchi hizi mbili fursa mbalimbali.
“ Utekelezaji wa mradi huu utafungua fursa za ajira kwa watanzania, kuchochea shughuli za kiuchumi kwa mikoa inayopita bomba hilo, pamoja na kufungua ukanda wa biashara wa kaskazini mwa Tanzania na Uganda pamoja na kuimarisha uhusiano katika soko la Afrika Mashariki” alifafanua Waziri Mahiga.
Katika hatua nyingine, Waziri Mahiga alisema kuwa kuhusu mgogoro wa nchini Burundi, kumekuwepo na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Rais Museveni pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa ili kuhakikisha amani inarejea nchini humo.
Katika ziara hiyo ya Rais Museveni nchini, atapokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Johm Magufuli ambapo atatembelea Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuangalia maboresho yaliyofanywa katika bandari hiyo, pamoja na Kiwanda cha kutengeneza Juisi cha Azam kilichopo Vingunguti jijini Dar es salaam
No comments:
Post a Comment