Polisi Waingilia Kati Mzozo wa Kanisa la Anglikana.......Wamzuia Askofu Mokiwa Kushiriki Ibada
Polisi wameingilia kati mvutano ndani ya Kanisa la Anglikana baada ya kumzuia Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dkt. Valentino Mokiwa kushiriki ibada ya kumsimika Askofu mpya wa Dayosisi ya Lweru.
Askofu Mokiwa amekuwa katika mvutano na Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania, Dkt. Jacob Chimeledya tangu alipotangaza kumvua uongozi wa Dayosisi ya Dar es Salaam, akidai mkuu huyo hakufuata utaratibu na kwamba hana mamlaka ya kuchukua uamuzi huo.
Aidha Askofu Mokiwa aliwasili makao makuu ya Dayosisi ya Lweru mjini Muleba mkoani Kagera na alitarajiwa kuungana na maaskofu wengine kumsimika Godfrey Mbelwa kuwa askofu mpya wa dayosisi hiyo.
Lakini taarifa zilizopatikana zimesema Askofu Mokiwa alichukuliwa na polisi na kuhojiwa katika kituo cha Muleba, kutokana na kuhofu kuwa kuwapo kwake kungeweza kusababisha vurugu katika ibada iliyokuwa iongozwe na Dkt. Chimeledya kutokana na mvutano uliopo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Augustino Ollomi,amesema kuwa jeshi hilo halikumkamata Askofu Mokiwa na kumhoji, badala yake amesema walichukua hatua haraka baada ya kupata taarifa za kiintelijensia kuhusu masuala ya usalama.
“Ni wajibu wetu kufuatilia, tulimuonya kuhusu suala la kuhudhuria ibaada kwa sababu kulikuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani lakini ilikuwa ni hiari yake kutohudhuria, huo utakuwa ni uamuzi wake,”amesema Ollomi.
Kamanda Ollomi amesema walimuita Askofu Mokiwa juzi saa moja usiku kwa ajili ya kumpa ushauri wa kutohudhuria sherehe hizo kwa kuwa mgogoro uliopo katika kanisa hilo ungeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
No comments:
Post a Comment