Mahakama Yafuta Kesi ya Mtuhumiwa wa Escrow
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemwachia huru Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA), Theophillo Bwekea, baada ya Jamhuri kuonyesha haina nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Bwekea alikuwa akituhumiwa kupokea rushwa ya Sh milioni 161.7 kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira.
Wakili wa Serikali, Odossa Olombe, alidai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respiciou Mwijage kwamba upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Hivyo aliomba kuondoa kesi hiyo chini ya kifungu cha sheria namba 98(a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) aya ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Hakimu Mwijage aliyakubali maombi ya upande wa Jamhuri na kuamuru mshtakiwa kuachiwa huru chini ya kifungu cha sheria namba 98(a) cha CPA.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka Januari 20, 2015.
Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai, awali akisoma mashtaka alidai kuwa mshtakiwa anatuhumiwa kupokea rushwa ya Sh 161,700,000 kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira, ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwamo kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kabla ya kufanya kazi REA, Theophillo alikuwa Wizara ya Nishati na Madini, kitengo cha kusimamia umeme, ambako anadaiwa alishiriki kutunga sera ya kampuni binafsi kuuza umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na ilipoanza kutumika, Kampuni ya kufua umeme ya IPTL ilikuwa ya kwanza kupata zabuni.
Wakili Swai, alidai Februari 12, 2014 katika Benki ya Mkombozi, mshtakiwa akiwa Mhandisi Mkuu wa REA, kwa rushwa alijipatia Sh milioni 161.7 kupitia akaunti namba 00410102643901 fedha ambazo ni sehemu ya zilizokuwapo katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Alidai fedha hizo aliingiziwa katika akaunti yake na Rugemalira ambaye ni mshauri binafsi wa kimataifa, Mkurugenzi wa VIP Engineering na alikuwa Mkurugenzi wa IPTL.
Fedha hizo zinadaiwa alipewa zawadi kwa kuwa alikuwa mmoja wa wajumbe walioandaa sera zilizoruhusu sekta binafsi kuuza umeme Tanesco.
Mshtakiwa huyo alikuwa nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa Serikali ama kutoka taasisi inayotambulika waliotakiwa kuwa na barua za utambulisho na kila mmoja kusaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 25.
No comments:
Post a Comment