Michezo: TFF Yasema Mechi ya Simba na Yanga iko palepale
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa mechi ya ligi kuu Tanzania Bara ya mzunguko wa pili kati ya Simba na Yanga iliyokuwa imepangwa kuchezwa Februari 18 mwaka 2017 iko palepale kwa kuwa bado halijafikiria kuibadili tarehe hiyo.
Hatua hiyo inatokana na tarehe hiyo kugongana na kalenda ya CAF ya michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika iliyotolewa hivi karibuni na kuipanga Yanga kucheza mchezo wa marudiano kati yake na Ngaya de Mbe ya Comoro kati ya tarehe 17, 18 na 19 mwezi Februari 2017.
Afisa Habari wa TFF Alfred Lucas amesema kuwa hadi sasa shirikisho hilo kupitia Bodi ya Ligi halijafikiria kufanya mabadiliko yoyote kwenye ratiba hiyo, na kwamba ratiba itaendelea kubaki kama ilivyo hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo.
"Ratiba imeshapangwa na haitabadilika, kila timu inajua itacheza lini, kuhusu ratiba ya CAF haiwezi kutuzuia kufanya mashindano yetu, kama kuna timu inacheza CAF inatakiwa ijipange, kila timu inatakiwa kuwa tayari wakati wowote ndiyo maana zinafanya matayarisho, zinaajiri makocha, zinasajili wachezaji , hiyo yote ni matayarisho kwahiyo sidhani kama watahitaji kupumzika na kutuharibia ratiba" Amesema Lucas
Jumatatu iliyopita Mtendaji Mkuu wa Bodi ya ligi Boniface Wambura akiwa kwenye kipindi cha 5Sports cha EATV, alisisitiza kuwa katika mzunguko wa pili wa ligi, ratiba haitakuwa tatizo, na kwamba haitabadilishwa badilishwa kwa kuwa katika upangaji wake kila kitu kilizingatiwa ikiwemo kalenda ya CAF.
No comments:
Post a Comment