Tanzania yachunguza madai ya Malawi kuwakamata wapelelezi wake
Serikali inafanya uchunguzi kuhusu tuhuma zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya Malawi kuwa vimewakamata ‘mashushu’ nane wa Tanzania wakijaribu kuingia kinyamela kwenye mgodi wa ‘uranium’.
Taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari nchini humo juzi zimedai kuwa watu hao nane walikuwa wapelelezi na kwamba walitaka kuingia kwenye mgodi huo kujaribu kuchunguza kama nchi hiyo inatengeneza ‘nyuklia’ katika eneo la Kayerekera. Ripoti iliyowekwa kwenye mitandao mbalimbali ya Malawi pia imedai kuwa watu hao waliingia nchini humo bila kuwa na nyaraka za kusafiria.
Akizungumzia madai hayo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga jana alifanya mahojiano na The Citizen na kueleza kuwa hakuwa na taarifa hizo lakini atazifuatilia kwa kina na kufanya uchunguzi kwani ni tuhuma kubwa na nyeti.
“Ndio ninasikia hilo kwa mara ya kwanza kutoka kwako. Hizi ni tuhuma kubwa, nitafuatilia kwa kina leo (jana) jioni kwa kuwasiliana na ubalozi wetu wa Malawi kufahamu kama wanafahamu lolote kuhusu hili,” Dk. Mahiga anakaririwa.
Hata hivyo, tofauti na ripoti zilizotolewa kwenye vyombo vya habari vya Malawi, Msemaji Msaidizi wa Polisi wa eneo la Karonga, George Mlewa alikana ripoti hizo akidai kuwa watu hao nane waliokamatwa wanachukuliwa kama wahamiaji haramu tu.
“Wakati tunaendelea na uchunguzi wetu kuhusu suala hili, naweza kusema kuwa ripoti hizo ni uvumi tu,” alisema Mlewa.
Chanzo: The Citizen
No comments:
Post a Comment