Upinzani na serikali wakutana DR Congo
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na vyama vya upinzani vinakutana katika mkutano ambao umeelezewa kama utakaovunja au kulijenga taifa hilo, lililoko maeneo ya maziwa makuu.
Taifa hilo linakumbwa na matatizo makubwa ya kisiasa ambayo yamechangia kuzorota kwa usalama nchini humo.
Muhula wa mwisho madarakani kwa rais Joseph Kabila, ulimalizika mapema mwezi huu, lakini uchaguzi mkuu umeahirishwa.
Wakati huohuo mapigano makali yalishuhudiwa hii leo kati ya vikosi kutoka jeshi la Jamuhuri ya kidemkrasia ya Congo FARDC, na waasi wa kikundi cha Maimai katika kijiji cha Moikene yapata kilomita sitini kusini mwaa mji wa Beni katika mkoa wa kivu ya kaskazini mashariki mwa DRC.
Duru za kuaminika zaeleza kuwa waasi wa Mai-Mai walishambulia ngome moja ya jeshi la congo FARDC mapema alfajiri na kuanza kurushiana risasi.
Walioshudia mapigano hayo wanasema kuwa yalichukuwa mda wa saa tano lakini hakuna anayejua idadi ya waliouawa wala kujeruhiwa.
Tangu mwanzo wa mwezi Oktoba mwaka wa elfu mbili na kumi na nne Beni ,imekuwa shamba la vita pamoja na mauaji, huku raia wa kawaida wakiathiriwa vibaya.
Kundi la waasi wa ADF kutoka nchini Uganda ndio linatajwa kuwa tishio kubwa katika maeneo hayo.
Licha ya majeshi ya serikali kujitahidi kukabiliana na wapiganaji kutoka makundi ya waasi ya ADF pamoja na Maimai, Hali ya usalama bado ni tete Beni.
Makundi hayo yamekuwa yakitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya wanavijiji, ambapo wahalifu huwavamia na kuanza kuwauwa kwa kutumia shoka ,mapanga pamoja na bunduki na kusababisha vifo vingi.
Maelfu ya wanavijiji pia wamelazimishwa kuhama makwao.
Hata hivyo jitihada za kupata maoni ya upande wa serekali pamoja na jeshi kuzungumzia mauaji hayo hapa Beni ziliambulia patupu.
No comments:
Post a Comment