Uporaji wa Kutumia Bunduki Watikisa Jiji la Mbeya
Wamiliki wa maduka, bodaboda na grosali jijini Mbeya wamekumbwa na hofu baada ya kuibuka kwa kundi la watu wanaodaiwa kuwa majambazi ambao wamekuwa wakipora fedha na pikipiki katika maeneo tofauti tangu mwishoni mwa Januari.
Mitaa iliyoonja adha ya wavamizi hao ni ya Mafiati, Mwanjelwa, Mabatini, Soweto na Mabanzini ambako vikundi hicho kilivunja maduka matano.
Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Dhahiri Kidavashari alisema wanashikilia watu watatu kuhusiana na matukio hayo.
Kamanda Kidavashari alisema upelelezi wa awali unaonyesha kundi hilo limetokea Tunduma mkoani Songwe na kwamba lilipokewa na wenyeji ambao huwaongoza katika uporaji huo.
‘’Mpaka sasa tunamsaka kijana anayeitwa Frank Senior au Frank Popo wa Mtaa wa Iyela kwa madai ya kuhusika kusaidia uhalifu huo,’’alisema.
Awali, mwenyekiti wa wa Chama cha Waendesha Bodaboda Kanda ya Soweto, Joseph Patrick alisema hivi karibuni kuna watu walifika eneo hilo saa 3:00 usiku wakawavamia madereva na kuwapora fedha, kisha wakavamia Mtaa wa Block Q walikopora pikipiki mbili.
Aliwataja walioporwa kuwa ni Saimon Nkwandi na Msafiri Jumanne. Patrick alisema waporaji hao pia walimpiga risasi dereva mwingine aliyemtaja kwa jina la Peter Hans baada ya kukataa kuwakabidhi pikipiki.
Mkazi wa Mafiati, Betweli Mwakitabu alidai waporaji hao walivamia grosari zaidi ya tano na kupora fedha kwa wamiliki na wateja. Tukio kama hilo lilitokea pia Mtaa wa Mabanzini.
No comments:
Post a Comment