Wabunge wacharuka matumizi ya fedha za wafadhili
Wabunge wameitaka Serikali kutoa maelezo ya dola 300 milioni za Kimarekani (sawa na Sh570 bilioni) zilizotolewa na wahisani kwa ajili ya kusaidia miradi ya afya, lakini hazijatumika.
Fedha hizo zilitolewa na Global Fund kwa ajili ya kugharamia miradi ya Ukimwi, malaria na kifua kikuu (TB) na zinatakiwa hadi kufikia Desemba mwaka huu ziwe zimeshatumika.
Mjadala huo ulizuka jana katika semina ya wabunge wa kamati tatu za Bunge kuhusu afya ya wanawake, watoto na vijana iliyoandaliwa na Umoja wa Mabunge ya Dunia (IPU) na Bunge la Tanzania.
Semina hiyo ilishirikisha Kamati ya Bajeti, Huduma na Maendeleo ya Jamii na ya masuala ya Ukimwi.
Akizungumza katika semina hiyo, mbunge wa viti maalumu (Chadema), Suzan Lyimo alisema bila kuwa na bajeti ya kutosha, malengo ya pambano dhidi ya Ukimwi hayawezi kufikiwa.
“Tunasikia kuna wadau wengi waliokuwa wanasaidia eneo hili wamejiondoa. Nataka kufahamu wanasemaje kuhusu hili?” alihoji.
Akijibu hoja hiyo, Marianna Balampama kutoka Kundi la Washirika wa Maendeleo (DPG), alisema wafadhili hawajajitoa kusaidia miradi hiyo. Alisema wafadhli hao kama Marekani na Global Fund wanaendelea kutoa misaada.
Hata hivyo, alisema muda wa dola 300 milioni za Kimarekani zilizotolewa na Global Fund unakaribia kuiisha, lakini hazijatumika.
Alisema kutokana na masharti mapya ya Global Fund, muda wa kutumika ukimalizika, kama hazijatumika hutakiwa kurudishwa.
Hali hiyo iliwafanya wabunge wengine kuanza kuguna na wengine kunong’ona. Kutokana na maelezo hayo, Deogratius Rutatwa, ambaye ni ofisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), aliiomba Serikali kuchukua hatua za haraka ili fedha hizo zisirudishwe.
Hata hivyo, Dk Nemes Irya kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) aliwatoa hofu wabunge kuwa fedha hizo haziwezi kurudi kwa wafadhili.
“Huwa fedha hizi zinakuja kwa mafungu kama tunavyotekeleza miradi,”alisema.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Serikali ilikuwa na mazungumzo na Global Fund ya jinsi ya kutumia kiasi hicho cha cha fedha hizo katika kuboresha miundombinu. Waziri Ummy alisema ameiam- bia Global Fund kuwa Serikali inataka iwe na uamuzi kwa asilimia 15 ya fedha zinazotolewa.
“Mwaka huu nimewambia Global Fund, kati ya hizo Dola 380 milioni za Kimarekani mnazotupatia, asilimia 15 nizitenge mimi. Niamue tunazitumiaje, wasitu lazimishe tuzitumie kwaajili ya Ukimwi na malaria tu, bali nizitumie kuboresha mifumo.” Ummy Mwalimu
No comments:
Post a Comment