Wabunge wazidi kupinga Wizara kuhamia Udom
Siku chache baada ya wabunge kueleza kutoridhishwa na Serikali kuhamia kwenye majengo ya Chuo Kikuu Dodoma (Udom), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii nayo imepinga hatua hiyo.
Kamati hiyo pia imeshauri Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), kuachana na utaratibu wa kupangia wanafunzi vyuo na ijikite kusimamia ubora wa elimu inayotolewa na vyuo vikuu nchini.
Mapendekezo hayo yametolewa bungeni mjini Dodoma na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2016.
Serukamba amesema kamati hiyo ya Bunge inaunga mkono Serikali kuhamia Dodoma, lakini utaratibu wa Wizara kuhamishia ofisi zao Udom siyo sawa.
Wizara ambazo zimehamishia ofisi zake Udom kutoka Dar es Salaam ni Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Katiba na Sheria; Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
No comments:
Post a Comment