Henrikh Mkhitaryan: Nyota wa Manchester United apata jeraha
Kiungo wa kati wa Manchester United Henrikh Mkhitaryan atakaa nje hadi baada ya Krismasi baada ya kuumia kifundo cha mguu wakati wa ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Tottenham Jumapili.
Raia huyo wa Armenia mwenye umri wa miaka 27 alichezewa visivyo na beki wa kulia wa Spurs Danny Rose na baada ya kupewa matibabu muda mrefu uwanjani, aliondolewa kwenye machela dakika ya 85.
Meneja wa United Jose Mourinho hata hivyo alisema jeraha hilo si mbaya sana.
"Inaonekana kama atakosa mechi kadha zijazo, lakini hatahitaji upasuaji. Twatumai atarejea siku ya Boxing Day," Mourinho aliambia MUTV.
Mourinho alikuwa awali ameeleza wasiwasi kwamba jeraha hilo lingekuwa mbaya lakini baadaye akasema watamkosa kwa "wiki kadha tu".
Atakosa mechi ya Jumatano ugenini dhidi ya Crystal Palace na mechi ya Jumamosi dhidi ya West Bromwich Albion.Huenda akarejea kucheza dhidi ya Sunderland mnamo 26 Desemba.
Mkhitaryan ndiye aliyewafungia United bao hilo la ushindi dhidi ya Tottenham uwanjani Old Trafford.
Alikuwa pia amewafungia wakati wa ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Zorya Luhanks katika Europa League Alhamisi.
Mkhitaryan alinunuliwa £26m kutoka Borussia Dortmund majira ya joto mwaka huu.
No comments:
Post a Comment