Mkuu Brigedi ya Nyuki JWTZ afariki dunia
KAMANDA wa Brigedi ya Nyuki ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Brigedia Jenerali Cyril Mhaiki, amefariki dunia katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania, Davis Mwamunyange, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, alisema jana kuwa, amepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Brigedia Jenerali Mhaiki aliyefikwa na mauti juzi.
Dk Shein kwa niaba yake na ya wananchi wote Zanzibar, alisema wamepokea kwa mshtuko, taarifa ya kifo cha Kamanda huyo hodari aliyetoa mchango mkubwa katika shughuli za ulinzi na usalama na maendeleo ya nchi.
Aidha, salamu hizo za rambirambi zilieleza kuwa Brigedia Jenerali Mhaiki ameacha pengo kubwa, si tu kwa familia yake, bali kwa Brigedi ya Nyuki, JWTZ na nchi kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa mchango wake hautosahaulika.
Alimuomba Mwamunyange kuzifikisha salamu hizo za rambirambi kwa wanafamilia, maofisa na wapiganaji wa vikosi vyote vya ulinzi na usalama.
Pamoja na hayo, salamu hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huku akimuomba Mwenyezi Mungu kumlaza mahala pema Kamanda huyo.
No comments:
Post a Comment