Aliyeongoza kamati ya Makinikia akumbwa katika kashfa ya Almasi na Tanzanite
Wakati kumbukumbu za ripoti za uchunguzi wa usafirishaji wa mchanga wa madini (makinikia) nje ya nchi zikiwa bado zinawatafuna watanzania walio wengi kuhusu hatma ya nchi yetu katika sekta ya madini baada ya taarifa kuonyesha tumeibiwa sana, kidonda hicho kimetonyeshwa upya jana baada ya kamati mbili za bunge kuwasilisha ripoti kuhusu biashara ya madini ya Almasi na Tanzanite.
Kamati ya iliyochunguza biashara ya madini ya Almasi imeongozwa na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu huku Kamati ya Tanzanite ikiongozwa na Mbunge wa Bukombe, Doto Mashaka Biteko.
Wakati wenyeviti wa kamati zote wakiwasilisha ripoti zao mbele wa Spika wa Bunge na viongozi wengine waandamizi wa serikali na vyombo vya ulinzi, wameonyesha namna serikali inavyopata hasara kutokana na kusainiwa kwa mikataba mibovu, rushwa, biashara za kupendeleana, maamuzi ya kukurupuka lakini pia na uzembe wa viongozi walioaminiwa kulinda rasilimali hiyo adimu.
Moja ya jambo lililowashtua watu wengi na pengine kuleta mfadhaiko, ni baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Almasi, Mussa Azzan alipokuwa akieleza moja ya sababu zilizosababisha serikali kupata hasara na kubambikiwa madeni ni kiongozi aliyekuwa akihusika na uhakiki wa madeni hayo kutokuwa makini.
Zungu alisema, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa Madini Nchini, Profesa Abdulkarim Hamis Mruma amelisababishia taifa hasara kwa kuruhusu madini yapotee kwa uzembe.
Prof. Mruma ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kwanza ya Makinikia iliyoundwa na Rais Magufuli alipohojiwa sababu za kusababisha hasara hiyo na serikali kubambikiwa madeni ambayo si halali alisema, nyaraka hizo za madini alizisaini bila kusoma.
Kamati ilipohoji kwanini kiongozi wa ngazi ya juu kama yeye anasaini nyaraka bila kuzisoma alisema kuwa alikuwa ametingwa na kukosa muda wa kusoma ripoti zilizoletwa kwake, lakini pia alikuwa anawaamini waliokuwa wakizileta ndio sababu hakusita kuzisaini.
Prof. Mruma alijizolea sifa nyingi alipowasilisha ripoti ya uchunguzi wa makinikia ambapo yeye na wajumbe wengine wa kamati walikuwa wakichunguza aina ya madini iliyokuwa katika mchanga huo. Katika ripoti yake alionyesha namna taifa linavyopoteza matrilioni fedha kutokana na usafirishwaji wa mchanga wa madini nje ya nchi.
Wengine walionaswa na kamati hizo ni waliokuwa Mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. Muhongo na William Ngeleja ambao wao kwa nyakati tofauti inadaiwa walitoa leseni za uchumbaji madini kwa kampuni mbalimbali mfano Tanzanite One kinyume na sheria.
Aakieleza zaidi Zungu alisema, kuna leseni moja ya madini ambayo serikali ilishauriwa na kamati nyingi kutoitoa, lakini Prof. Muhongo siku chache baada ya kuingia madarakani alitoa leseni hiyo.
Mwingine anayetuhumiwa kuisababishia serikali hasara ni pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani wakati akifanyakazi katika Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambapo kamati imeeleza kuwa alishindwa kusimamia wajibu wake vizuri na kulisababishia taifa hasara.
Aidha, miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na kamati hizo, ni serikali kuwachukulia hatua watumishi wote waliohusika kwa namna moja ama nyingine katoka kulisababishia taifa hasara.
Lakini pia kamati zimependekeza kupitiwa kwa mikataba ya kampuni za uchimbaji madini kwani biashara hiyo imekumbwa na rushwa na uongo, hali inayosababisha serikali kupata hasara.
No comments:
Post a Comment