Utetezi wa Serikali Kuhusu kesi ya mamlaka ya wakuu wa mikoa na wilaya Kuwaweka Watu Mahabusu kwa saa 48
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), amewasilisha utetezi dhidi ya kesi ya kupinga mamlaka ya wakuu wa mikoa na wa wilaya kuamuru watu kuwekwa ndani kwa saa 48, kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Pamoja na maelezo ya utetezi, Serikali pia imewasilisha pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo ikiiomba Mahakama iitupilie mbali hata kabla ya kuisikiliza.
Kesi hiyo ya Kikatiba namba 16 ya mwaka 2017 imefunguliwa na mwanasheria wa kujitegemea, Jebra Kambole dhidi ya AG, akidai ni kutokana na kukithiri kwa matukio ya wakuu wa mikoa na wilaya kuamuru watu kuwekwa mahabusu kwa saa 48.
Mwanasheria huyo anahoji uhalali wa vifungu vya 7 na 15 vya Sheria ya Tawala za Mikoa Sura 97 ilivyorekebishwa mwaka 2002 vinavyowapa wakuu hao wa mikoa na wa wilaya mamlaka hayo, akidai vinatumiwa vibaya bila kujali mipaka, sababu, wala bila fursa ya kumsikiliza.
Kambole ambaye anawakilishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), anaiomba Mahakama itamke kuwa vifungu hivyo vinakiuka haki za binadamu zinazotolewa na Katiba ya nchi.
Amezitaja haki zinazokiukwa kutokana na utekelezaji wa vifungu hivyo kuwa ni uhuru wa kujieleza, usawa mbele ya sheria, utu na haki ya mtu kuwe huru na kwenda mahali kokote atakako kinyume cha ibara za 12, 13(6)(a)(b)(e), 15 na 29 (1) za Katiba.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika majibu yake amesema vifungu hivyo havikiuki haki hizo zinazotolewa na Katiba ya nchi bali vinaenda sambamba na Katiba.
Pia, ameweka pingamizi la awali akiiomba mahakama iitupilie mbali kesi hiyo.
Katika sababu zake za pingamizi la awali, anadai kesi hiyo haileweki na ni batili kisheria kwa kuwa inakiuka kifungu cha 4 na cha 8 cha Sheria ya Utekelezaji wa Wajibu na Haki za Msingi na kwamba haina maana na ni ya kuudhi.
Pia, anadai kiapo kinachounga mkono hati ya maombi ya faragha hakina mashiko kwa sababu kinakiuka Amri XIX ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai.
Katika maelezo yake ya utetezi, pamoja na mambo mengine anadai vifungu hivyo vinatoa utaratibu mzuri kwa wakuu wa mikoa na wa wilaya wa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Anabainisha kuwa, vifungu hivyo vinawapa wakuu wa mikoa na wa wilaya mamlaka kwa mambo yanayohusu uvunjifu wa amani na utulivu kwa umma pale uvunjifu huo unapokuwa hauwezi kuzuiliwa kwa njia nyinginezo zaidi ya kumweka kizuizini mtu husika.
Anadai makosa yote yanachunguzwa, yanashtakiwa na kushughulikia kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, isipokuwa tu pale ambapo sheria inaelekeza vinginevyo.
AG anadai masuala yanayohusu dhamana chini ya Sheria ya Tawala za Mikoa yanaongozwa na Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai.
No comments:
Post a Comment