Mwanzilishi wa Jamii Forums Jana Hakufikishwa Mahakamani.......Polisi Walivamia Ofisi zake na Kufanya Upekuzi
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limevamia ofisi za mtandao wa Jamii Forums (JF) na kufanya upekuzi na kuondoka na nyaraka za usajili wa Jamii Media ikiwemo cheti cha mlipa kodi, cheti cha BRELA, leseni ya biashara, n.k..
Askari hao walivamia ofisi hizo jana mchana wakiwa wamefuatana na na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao huo, Maxence Melo, wakafanya upekuzi na kuwahoji baadhi ya wafanyakazi.
Baada ya kufanya upekuzi ndani ya ofisi hiyo walielekea nyumbani kwa mkurugenzi huyo, kufanya upekuzi kabla ya kumrudisha rumande kwa vile hakufikishwa mahakamani.
Melo alikamatwa juzi na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi ambako aliwekwa selo.
Anakabiliwa na mashtaka ya kuzuia upelelezi wa makosa ya mtandao kwa kushindwa kutoa taarifa binafsi za watumiaji wa mtandao wa Jamii Forums ambazo polisi walizihitaji.
Taarifa iliyotolewa jana na mtandao huo iliwataka watumiaji wake kutokuwa na hofu yoyote na kwamba Jamii Forums haina server Tanzania wala Africa .
"Tunaomba umma utambue kwamba Jamii Media haina servers wala min-server ofisini kwake, nchini Tanzania wala Afrika. Pili, tunaomba watumiaji wa JamiiForums.com wasitiwe wasiwasi juu ya usalama wa taarifa zao.
"Teknolojia tunayoitumia (encryption) kumsajili mtumiaji wa JamiiForums.com haituwezeshi kumfahamu mtumiaji yeyote labda yeye akubali kwa hiari yake kujiweka wazi mtandaoni." Ilieleza taarifa hiyo
No comments:
Post a Comment