NSSF Yaanza kutekeleza Agizo la Rais Magufuli La Kujenga Viwanda Badala ya Majengo
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika kuhakikisha inatatua changamoto ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana umeamua kuachana na uwekezaji wa majengo makubwa na badala yake imeanza kuelekeza nguvu katika kufufua viwanda.
NSSF imeazimia kuunga mkono malengo ya Rais John Magufuli ya kukuza uchumi kwa kufufua viwanda na kwa kuanzia mfuko huo umeamua kufufua viwanda vya usagishaji vilivyokuwa katika mikoa ya Iringa, Mwanza, Dodoma na Morogoro.
Hivi karibuni, Rais Magufuli aliagiza mifuko hiyo kuachana na ujenzi wa majengo badala yake ikijike katika ujenzi wa viwanda.
Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bathon Mmuni alisema hayo mjini Morogoro katika mkutano uliowakutanisha wadau wa mfuko huo kutoka taasisi za Serikali na binafsi ili kujadili masuala mbalimbali kuhusiana na mfuko huo.
“Lazima fedha wanazochanga wanachama zizalishe haziwezi kukaa tu, uwekezaji ni moja ya faida kwa mwanachama wetu, hivyo lazima tubadilishe uwekezaji ili kupata faida,” alisema.
Mmuni alisema kwa muda mrefu nchi imekuwa na changamoto ya ajira hasa kwa vijana, hivyo wameamua kufanya uwekezaji upande mwingine ikiwa katika kufufua na kujenga viwanda.
Alisema ili kumsaidia Rais Magufuli katika kukuza uchumi, mbali na usagishaji wanaelekeza nguvu katika viwanda vya sukari.
Alisema mfuko huo pia unalenga kuwawezesha Watanzania kupata ajira, hususani kwa vijana na kwa kuanzia shirika litaanza na ujenzi wa kiwanda cha sukari katika eneo la Mkulazi kwa kushirikiana na Mfuko wa Pensheni wa PPF kupitia kampuni tanzu ya Mkulazi Holding.
Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa NSSF, Tikyeba Alphonce alitaja baadhi ya changamoto zinazoukabili mfuko huo kuwa ni baadhi ya waajiri kuchelewa kuwasilisha fedha za wanachama.
No comments:
Post a Comment