Mazombi Yavamia ofisi za CUF Zanzibar......Yapora Mali na Kujeruhi Watu
Watu wasiojulikana maarufu kama mazombi wameivamia ofisi ya Chama cha Wananchi (CUF) katika Jimbo la Dimani Wilaya ya Magharibi B.
Katika tukio hilo lililotokea saa 6.30 usiku wa kuamkia jana, inadaiwa mazombi hayo yalipora mali, kujeruhi watu na kuwateka wengine wa nyumba jirani na ofisi hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo huku CUF wakitaka uchunguzi uanze mara moja kuwabaini wahalifu.
“Ni kweli taarifa tunazo za watu kuvamia ofisi hiyo ya CUF na kuwapiga pamoja na kuwahujumu watu na huo ni uharamia unaoripotiwa mara kwa mara,” alisema Kamanda Ali.
Katika tukio hilo, watu hao walioripotiwa kuwa na bunduki na silaha za jadi kama mashoka, mapanga, mashanuo, chupa, spoku za baiskeli na nyundo, walidaiwa kuvunja milango ya jengo la ofisi hiyo katika kijiji cha Bweleo kabla ya kutembeza kipigo kwa majirani na kuondoka na vitu kadhaa.
Katika tukio hilo inadaiwa mazombi walitoweka na watu kadhaa akiwamo Mwenyekiti wa CUF Tawi la Bweleo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazee wa chama hicho Wilaya ya Magharibi, Juma Ali Juma.
Akilaani tukio hilo, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa CUF, Salim Abdallah Bimani alisema, “Huu ni uvunjifu wa amani na tunataka Rais John Magufuli iwapo anayo nia ya dhati afuatilie hujuma hiyo ambayo watekelezaji wake wanajulikana lakini hawakamatwi.”
Bimani alisema, “Mazombi wameshawapiga sana wananchi hasa wafuasi wa CUF ambao hawana hatia, wengine mpaka walipo-teza maisha, wameshawapiga watu na kuwajeruhi vibaya na pia kuwaibia watu mali zao na hatuoni hatua yoyote ikichukuliwa.”
Bimani alisema, “Tunamwambia Rais Magufuli kwa mujibu wa Katiba yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuwalinda raia wote wa nchi hii, achukue hatua.”
Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF, Pavu Juma Abdalla aliwataja waliojeruhiwa kutokana na vipigo vikali kuwa ni pamoja na Juma Shani Mwita, Ali Saleh Shani, Kessi Khatib na Ame Mahmoud, wote wakazi wa Bweleo.
Pavu alisema kuwa tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Fumba na wahusika walipewa RB Na.18/2017.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo inadaiwa kuwa miongoni mwa mali walizotoweka nazo ‘mazombi’ kutoka ndani ya ofisi hiyo, ni simu nne, fedha taslimu Sh300,000, viti 20, kifaa cha kudhibiti umeme, friji na bendera na mlingoti wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali alisema, “Ni kweli taarifa tunazo za watu kuvamia ofisi hiyo ya CUF na kuwapiga pamoja na kuwahujumu watu na huo ni uharamia unaoripotiwa mara kwa mara.”
Nassir alisema, “Pamoja na juhudi tunazozichukua ili kuukomesha kwa kushirikiana na vikosi vingine, inaonekana hauwezi kuondoka kwa mara moja.”
Alisema kuwa jana walifanikiwa kuwashikilia watu wawili ili kusaidia polisi wakati ambapo jeshi hilo likiendelea na upelelezi.
Shambulio hilo lilitendeka saa chache baada ya makamu mwenyekiti mstaafu wa CUF, Juma Duni Haji na Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea kuwasili Dimani ili kuendelea na kampeni za kumnadi mgombea wao, Abdulrazaq Khatib Ramadhan.
No comments:
Post a Comment