UINGEREZA: Mahakama yaamuru Bunge kuhusishwa kuamua kama Serikali inaweza kuanza mchakato wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya(EU).
Mahakama ya Juu nchini Uingereza imeamua kuwa ni lazima wabunge nchini humo wajadili na kupigia kura mchakato wa nchi yao kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.
Uamuzi huu wa Mahakama unamaanisha kuwa Waziri Mkuu Theresa May hawezi kuanza mazungumzo ya kujiondoa kwenye umoja huo kabla ya suala hili kujadiliwa na kupigiwa kura na wabunge.
Uingereza imepewa hadi mwisho wa mwezi Machi kuanza mchakato wa kujiondoa kwenye Umoja huo baada ya raia wa nchi hiyo mwaka uliopita, kujiondoa kuwa wanachama baada ya kufanyika kwa kura ya maoni.
Hata hivyo, Mahakama hiyo imeamua kuwa Mabunge ya Scotland, Wells na Ireland Kaskazini hayana umuhimu wa kujadili na kulipigia kura suala hili.
Baadhi ya wanasiasa nchini Uingereza wamekuwa wakisema serikali kuanza mchakato huo bila ya kuihusisha bunge, ni kinyume cha miiko ya kidemokrasia nchini humo.
Serikali ya Uingereza ilikwenda katika Mahakama ya Juu kutaka Majaji watoe uamuzi kuwa ina mamlaka ya kuendelea na mchakato huo lakini hata kabla ya uamuzi huu, ilisema itaheshimu uamuzi wa Mahakama.
Majaji nane waliamua kuwa mchakato huo uanzie Bungeni huku watatu wakipinga.
No comments:
Post a Comment