Rais mpya wa Gambia kurejea nyumbani siku ya Alhamisi
Rais mpya wa Gambia Adama Barrow anatarajiwa kurejea nyumbani siku ya Alhamisi, baada ya kiongozi wa zamani Yahya Jammeh kuondoka nchini humo kwenda kuishi nchini Equitorial Guinea.
Mai Fatty msemaji wa rais Barrow ambaye amekuwa akiishi nchi jirani ya Senegal alikoapishwa, ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP kuwa rais huyo mpya atarejea nyumbani ili kuanza rasmi majukumu ya kuliongoza nchi hiyo.
Aidha, Fatty amesema rais Barrow anatarajiwa kuwasili jijini Banjul Alhamisi mchana akitokea jijini Dakar.
“Ndio, kesho mchana atawasili,” Fatty ameliambia Shirika la AFP.
Barrow aliyeshinda Uchaguzi wa mwezi Desemba mwaka uliopita, alisema hawezi kurejea nyumbani hadi pale atakapopewa idhini na jeshi la Umoja wa nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ambalo kwa sasa lipo jijini Bajul kuhakikisha kuwa kuna usalama hasa katika Ikulu na makaazi ya rais.
Maelfu ya raia wa Gambia ambao walikimbilia katika nchi jirani ya Senegal, wameanza kurejea nyumbani baada ya Jammeh kuondoka wiki iliyopita.
Jammeh alilazimika kuondoka nchini humo baada ya kutishiwa kuondolewa kwa nguvu na jeshi la ECOWAS lakini pia baada ya marais wa Mauritania na Guinea, kuingilia kati mzozo huo na kumshawishi kuondoka nchini humo na kukabidhi madaraka.
No comments:
Post a Comment