Sumaye: Rais Magufuli Anatekeleza Sera za CHADEMA
Wakati Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli akitekeleza masuala mbalimbali aliyowaahidi Watanzania, ikiwa ni pamoja na kurejesha uwajibikaji na kupambana na ufisadi, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema hashtushwi na utendaji huo wa rais, kwani amekuwa akitumia baadhi ya hoja na mikakati ya Chadema kuongoza nchi.
Akizungumza wakati wa kumnadi mgombea wa udiwani katika kata ya Isagehe wilayani Kahama, Sumaye ambaye alijiunga Chadema Agosti mwaka juzi baada ya kuachana na CCM, alisema mengi anayofanya rais ni sera za Chadema ila chama hicho cha upinzani hakikuwa na sera ya kubana fedha.
Hata hivyo, Sumaye ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema hakuweka wazi hoja na mikakati ya Chadema inayotekelezwa na Rais Magufuli ambaye tangu aingie madarakani ameweka msimamo katika suala la kubana matumizi ya Serikali, kudhibiti watumishi hewa na safari za ndani na nje zisizo na tija na rushwa.
Katika mkutano huo ambao pia Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa alihutubia, Sumaye alisema kama wananchi, wangemchagua Lowassa kuwa Rais, angewaletea neema ya hali ya juu kwa kuwa angekuwa na misingi katika sera anazozitekeleza.
“Mmechagua Rais mzuri (Magufuli), lakini anafuata sera za chama chetu (Chadema) ambazo tungezitumia kama tungekuwa madarakani. Wananchi wa Kanda ya Ziwa mnatakiwa kumtumia Rais Magufuli ili kufanikisha malengo yetu,” alisema huku akisisitiza kuwa hata Lowassa wananchi wangeweza kumtumia kufanikisha malengo yao.
Huku akimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, John Luzinga, Sumaye aliwataka wananchi kutofanya makosa tena ya kuichagua CCM, ili wasije kujuta kwa maelezo kuwa watalazimika kuchagua diwani mwingine mwaka 2020.
Alisema Chadema kinaendeshwa kwa kufuata misingi ya demokrasia, huku akikosoa vyama kubanwa wakati nchi iriuridhia mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Akizungumzia sababu za kuhama CCM, alisema kulitokana na nchi kukumbwa na hali mbaya ya uchumi sambamba na kukosekana kwa utawala bora.
“Serikali pamoja na kubana matumizi, hali ya uchumi imekuwa mbaya. Inatakiwa kuachia fedha ili kuwafikia wananchi waweze kumudu ugumu wa maisha unaowakabili kwa sasa. Haiwezekani kila Serikali isijifunze katika hili wakati hata wataalamu wanazungumza na kushauri masuala mbalimbali,” alisema Sumaye.
Alisema kitendo cha halmashauri tatu za wilaya ya Kahama kuongozwa na CCM, huku diwani mmoja tu ndio akiwa wa Chadema, kitawafanya wananchi hao kukosa watu sahihi wa kuwasemea mambo yao.
Uchaguzi katika kata hiyo utafanyika Januari 22 sambamba na kata nyingine 21 katika maeneo mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment