Rais Magufuli kupokea taarifa vyeti feki LEO
Rais Magufuli kupokea taarifa vyeti feki LEO
RAIS John Magufuli leo anatarajiwa kupokea taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma katika Ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma.
Taarifa iliyotolewa jana na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais katika Ikulu Ndogo ya Chamwino Dodoma, Jaffar Haniu ilisema taarifa hiyo itawasilishwa kwa Rais Magufuli na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki.
Zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma liliendeshwa na Serikali kuanzia Oktoba, 2016.
Hivi karibuni wakati akifungua rasmi nyumba mpya za makazi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Rais Magufuli alisema anasubiri ripoti kuhusu watumishi wa umma wenye vyeti feki wapatao 9000.
“…Kwa hiyo mnaweza mkaona shida zilizopo katika nchi hii, huku wafanyakazi hewa karibu 19,000, wanafunzi hewa ni zaidi ya 56,000, kila mahali unapokwenda ni matatizo, lakini ni lazima niyatatue matatizo kwa sababu mlinichagua kwa ajili hiyo,” alisisitiza Rais katika hotuba yake hiyo.
Waziri Masauni: Waliolipua Bomu Nyumba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar ni Viongozi wa CUF
Waziri Masauni: Waliolipua Bomu Nyumba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar ni Viongozi wa CUF
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema viongozi waandamizi wa chama cha wananchi (CUF) ndiyo walihusika na tukio la kulipua bomu katika nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar baada ya kufanyika uchaguzi mkuu
Mhe. Masauni alieleza hayo Bungeni Jijini Dodoma jana pindi alipokuwa akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Gandu kupitia tiketi ya (CUF) visiwani Pemba, Mhe. Othuman Omary Hajji alipotaka kujua kwanini mpaka leo hajizachukuliwa hatua stahiki kwa wafuasi wa CCM waliochoma nyumba za wanachama wa CUF huko visiwani Tumbatu, huku akidai serikali iliyopo madarakani siyo halali ni haramu kwa kuwa Jeshi la Polisi lilichangia kumuweka madarakani Dkt. Ali Mohamed Shein.
"Ni kweli baada ya uchaguzi mkuu baadhi ya vyama vya upinzani ikiwemo chake, viongozi walijitokeza kuhamasisha wananchi kufanya mambo yanayokiuka sheria za nchi yetu.
"Kuna matukio mbalimbali yalijitokeza ikiwemo kuchomwa moto nyumba, kuchoma mashamba, kurusha mabomu ikiwemo nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi wa Zanzibar ambayo kwa uchunguzi uliofanyika mpaka sasa, watu waliokamatwa kwa kuhusika urushaji bomu katika nyumba ya Kamishna ni viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF)". Alisema Masauni
"Kuna matukio mbalimbali yalijitokeza ikiwemo kuchomwa moto nyumba, kuchoma mashamba, kurusha mabomu ikiwemo nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi wa Zanzibar ambayo kwa uchunguzi uliofanyika mpaka sasa, watu waliokamatwa kwa kuhusika urushaji bomu katika nyumba ya Kamishna ni viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF)". Alisema Masauni
Pamoja na hayo, Masauni alisema Jeshi la Polisi limeshakamilisha uchunguzi wake na jalada la mashtaka lipo kwa DPP muda wowote kuanzia sasa litapandishwa Mahakamani ili sheria ichukuliwe.
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Atiwa Mbaroni
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Atiwa Mbaroni
Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, kwa tuhuma za kumshambulia mwanamke mmoja na kumsababishia maumivu makali mwilini.
Msambatavangu, ambaye alikuwa miongoni mwa wanaCCM waliofukuzwa uanachama katika Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho uliofanyika mwezi Machi, alikamatwa jana mchana
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Julius Mjengi, alisema kuwa kiongozi mstaafu anatuhumiwa kutenda kosa hilo wiki iliyopita.
Akifafanua, Kamanda Mjengi alibainisha kuwa kiongozi huyo alitenda kosa hilo akiwa na wenzake ambao asingeweza kuweka majina yao hadharani kwani wanaendelea kuwatafuta.
"Ni kweli tunamshikilia Jesca Msambatavangu, tumemkamata leo(jana) saa nane mchana na tunaendelea na uchunguzi dhidi yake,"alisema Mjengi na kuongeza:
"Jesca pamoja na wenzake wanatuhumiwa kumshambulia mwanamke mmoja mkazi wa Kibwabwa, walimshambulia na kisha kumchoma sindano ambayo mwanamke huyo hajui ni ya kitu gani," alisema Mjengi.
Alipohojiwa zaidi, Mjengi alikataa kuweka wazi jina la mwanamke na idadi ya watuhumiwa wengine kwa maelezo kuwa kufanya hivyo kunaweza kuharibu upelelezi unaoendelea.
CUF Lazima Kuchafuke....Wabunge Upande wa Maalim Wamepanga Kufanya Usafi Ofisi Kuu, Kambi ya Lipuma Imejipanga Kuwazuia
CUF Lazima Kuchafuke....Wabunge Upande wa Maalim Wamepanga Kufanya Usafi Ofisi Kuu, Kambi ya Lipuma Imejipanga Kuwazuia
Wapinzani wawili katika mgogoro wa uongozi wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Profesa Ibrahim Lipumba sasa wamefikia pabaya baada ya kuamua kupambana kuichukua ofisi ya makao makuu iliyopo Buguruni.
Kwa sasa ofisi hiyo inatumiwa na Profesa Lipumba, ambaye uamuzi wake wa kurejea madarakani mwaka mmoja baada ya kujiuzulu uenyekiti na nyadhifa nyingine zote, unapingwa na kundi lililopanga kuzichukua ofisi hizo Jumapili.
Jana, kundi linalompinga Profesa Lipumba lilitangaza kuwa litakwenda ofisi hizo Jumapili kwa ajili ya kusafisha “kila kitu ambacho hakitakiwi kiwepo”, lakini mwenyekiti huyo amesema ameshajiandaa kukabiliana nao na ameripoti suala hilo polisi.
Profesa Lipumba alisema hayo jana, ikiwa ni siku moja tangu Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limtake ajitokeze kuzungumzia kitendo cha walinzi wa CUF kuwashambulia waandishi wa habari waliokuwa kwenye mkutano ulioandaliwa na viongozi wa chama hicho Kinondoni.
Profesa Lipumba alikuwa akiwajibu wabunge wa CUF wanaomuunga mkono Maalim Seif waliowaambia wanahabari katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana kuwa wamepanga kwenda ofisi za Buguruni Jumapili ijayo na wataungana na wanachama wengine kufanya usafi.
“Tulianza kufanya usafi soko la Buguruni, tukamalizia katika ofisi yetu. Kwa hiyo katika hali nzuri, hatuhitaji wabunge wasumbuke kufanya usafi siku hiyo,” alisema Profesa Lipumba
Profesa Lipumba alisema watu hao hawana nia ya dhati ya kufanya usafi, bali wamepanga kufanya vurugu katika ofisi hizo kwa kushirikiana na watu wa chama kingine cha upinzani.
“Wanataka kuleta vurugu ili CUF ionekane na taswira mbaya kwa Watanzania. Naomba wanachama waepuke mtego huu, namshauri (Mbunge wa Temeke, Abdallah) Mtolea akafanye usafi huo Temeke mbona kuna masoko mengi tu machafu?” alisema.
Awali mjini Dodoma, wabunge wanaomuunga Maalim Seif walisema watakwenda na vifaa vya usafikuondoa kila uchafu watakaoukuta
“Wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao hawamkubali Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti, wameamua kwenda kufanya usafi kwenye ofisi zao za Buguruni, ofisi kuu ya CUF Buguruni,” alisema Mtolea akiwa ameambatana na wabunge wenzake katika mkutano na waandishi uliofanyika chumba cha habari cha Bunge.
“Na hatua hii imekuja baada ya kuona ofisi ile inatumika vibaya. Imekuwa ndio kijiwe cha wahuni kupanga matukio ya kihalifu. Kwenda kuvamia mikutano, kwenda kuwavamia watu na kadhalika. Sasa sisi kama wanachama tumeona hatuwezi kuiacha hali hiyo iendelee.”
Aliwataka wanachama kutoka maeneo ya Dar es Salaam, Pwani na mikoa mingine wafike kufanya usafi huo.
Alipoulizwa aina ya uchafu wanaoenda kuuondoa, Mtolea alijibu “ni kitu chochote ambacho hakiko mahali pake” na kwamba hata Profesa Lipumba hayuko mahali pake.
“Tangu Msajili amtambue Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti, hatujawahi kwenda katika ofisi yetu ya Buguruni, matokeo yake ofisi hiyo imekuwa na uchafu mwingi na kuwa pango la wahuni,” alisema Mtolea.
Alipoulizwa uwezekano wa kutokea vurugu, Mtolea alisema hawajiandai kufanya fujo, bali kufanya usafi.
Kuhusu kesi iliyopo mahakamani kuhusu mgogoro huo, alisema ile inapinga msajili kumtambua Lipumba na haizuii kusafisha ofisi yao.
Alisema hawaendi kuteka ofisi hizo, bali wanakwenda kwenye ofisi zao hivyo hawahitaji kuomba ruhusa kwa mtu yeyote.
“Ofisi ni chafu, sisi tunataka tukaisafishe kwa sababu imekuwa sehemu ya kupanga mipango mibaya kwa mustakabali wa chama,” alisema.
Akiweka msisitizo wa jibu hilo, Mbunge wa Chambani, Yusuf Salim Hussein alisema hakuna silaha ya moto inayoshinda nguvu ya umma.
Awali, wabunge hao walitoa tamko la kuunga mkono tamko la TEF kuhusu kulaani kitendo cha wafuasi wa Profesa Lipumba kuwashambulia waandishi wa habari.
Mnadhimu wa chama hicho na Mbunge wa Malindi, Ally Salehe alisema TEF imetoa tamko zito la kutaka waandishi wa habari kufanya kazi kwa usalama na uhuru.
“Na isiwe TEF tu, tunataka watu wote waliokerwa na tukio hilo watoe tamko la kulaani,” alisema.
Kuhusu tamko la TEF, Profesa Lipumba alisema atatoa tamko kuhusu suala hilo ifikapo leo.
“Mimi ni muumini wa demokrasia. Hapa ninavyoongea na wewe nipo katika hatua ya mwisho ya kumalizia kuandika barua kuelekea TEF ambayo itafika kati ya leo (jana) jioni au kesho,” alisema.
Hata hivyo, alisema mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano kwa umma, Abdul Kambaya alitoa tamko kuhusu tukio hilo.
Katika tamko lake, Kambaya alisema mmoja wa watu walioshiriki kushambulia mkutano ni mlinzi wao na kwamba alikuwa katika doria kudhibiti wanachama wanaofanya mikutano hotelini.