Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Agundua Madudu 5 Mirandi ya Ujenzi NSSF
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini kasoro katika mambo matano baada ya kufanya ukaguzi wa hesabu za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Ripoti ya CAG imekuja wakati wakurugenzi sita, mameneja watano na mhandisi mmoja wakiwa wamesimamishwa kazi tangu Julai mwaka jana kupisha uchunguzi.
Ripoti hiyo iliwasilishwa bungeni Aprili 13 mwaka huu, ikiwa ni siku chache tangu CAG, Profesa Mussa Assad aikabidhi kwa Rais John Magufuli.
Kasoro zilizobainika katika mfuko huo ni kiwango cha chini cha ukaliwaji wa majengo, usimamizi na udhibiti wa mikopo ya vyama vya ushirika vya akiba na mikopo, udhaifu katika uwekezaji wa ardhi.
Ripoti hiyo inabainisha kasoro katika Shamba la Dungu na mradi wa uwekezaji Tuangoma na kasoro nyingine ni katika mkataba wa mshauri katika ununuaji wa Pan Africa Energy Limited kwa Sh551.61 milioni.
Ripoti inaonyesha kuwa NSSF imewekeza kwa kiasi kikubwa katika majengo ya kupangisha kwa wateja kama vile hoteli, kampuni, watu binafsi na kutumia sehemu nyingine ya majengo hayo kama ofisi zake.
Imegundulika kuwa, kiwango cha upangaji katika majengo tisa ya uwekezaji kilikuwa chini ya kusudio la kiwango cha soko cha asilimia 80. Ripoti inaonyesha kuwa kiwango cha upangaji kilikuwa kati ya asilimia 0 na 43.
Rasilimali hizo za uwekezaji katika majengo zinajumuisha hoteli ya Mwanza, Kigoma, jengo jipya la biashara la Old Moshi -Arusha, jengo jipya la biashara la Kaloleni (Arusha), jengo jipya (Kahama), Njiro (Arusha), jengo kubwa la kibiashara Kilimanjaro, Mafao House (Ilala) na jengo kubwa la kibiashara la Morogoro.
Mbali na hali hiyo CAG amebaini kuwa NSSF ilisimamisha kutoa mikopo kwa wanachama wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo Juni, 2016 ili kuimarisha usimamizi na kuhakikisha kuwa kuna ukusanyaji wa marejesho ya mikopo.
Hata hivyo, mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamisha utoaji, ilikuwa na mapungufu ikiwamo mikopo ya Sh1 bilioni iliyotolewa kwa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo zaidi ya kiwango cha ukomo.
Ripoti inaonyesha NSSF ilitoa Sh21.3 bilioni kwa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Bunge (National Assembly Saccos) na Sh2.2 bilioni kwa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Jumuiya ya Ndugumbi (Ndugumbi Community Saccos).
Utoaji huo wa mikopo ulizidi kiwango cha ukomo kwa Sh1 bilioni, lakini menejimenti ya NSSF ilieleza kwamba mikopo kwa wanachama wa Bunge ilitolewa kama mpango maalum wa kuvutia wanachama wapya kwenye mfuko.
Pia, kuna vyama vya ushirika vya akiba na mikopo vilivyopewa zaidi ya asilimia 50 ya mali zote ilizonazo.
Pia, CAG ameeleza kuwa ushuru wa stempu ulikuwa haujalipwa kwa vyama vinne vya ushirika ambavyo vilipewa mikopo.
Vyama hivyo ni Masoko Madogo Madogo ambacho hakijalipa Sh500 milioni, Ngima (Sh500 milioni), Mafanikio (Sh490 milioni) na Mount Meru (Sh260 milioni).
Udhaifu uliogundulika kwenye Uwekezaji wa Ardhi
Kwa mujibu wa CAG, taarifa za fedha za NSSF zilionyesha kuwa iliwekeza kwenye viwanja (Benki ya Ardhi) kwa thamani ya Sh97.2 bilioni, lakini imebainika kuwepo na mapungufu katika ununuaji na uwepo wa ardhi zilizonunuliwa.
Ripoti inaonyesha kulikuwa hakuna mipango na upembuzi yakinifu kuhalalisha sababu za kuwekeza katika rasilimali kinyume na aya ya 3.3 ya Sera ya Uwekezaji ya NSSF ya mwaka 2012 inayolitaka shirika hilo kuwekeza rasilimali zake katika miradi inayolipa zaidi ili kuweza kunufaisha wanachama wake.
“Sikuweza kupata hati ya umiliki ya viwanja/mashamba vinne kwa sababu vipo katika mzozo wa umiliki. Viwanja hivi vilikuwa ni Nunge Beach kilichopo Bagamoyo chenye ukubwa ekari 67.35, kiwanja namba 146/4 Barabara ya Old Moshi kilichopo Halmashauri ya jiji Arusha, Clement Mabina Farm Bugando Magu na kiwanja namba 98 Barabara ya Nyerere (Pugu) Temeke chenye mita za mraba 8,825,” inaeleza ripoti ya CAG.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mfuko uliingia mkataba na Halmashauri ya jiji la Mwanza kwa ajili ya kununua viwanja 692 (viwanja 405 eneo la Kiseke na 287 Bugarika) kwa Sh1.89 bilioni.
Hata hivyo, ni viwanja 156 tu vilielekezwa Kiseke; wakati hakuna kilichoelekezwa upande wa Bugarika.
Pia, imesema kulikuwa na shamba namba 113 lililonunuliwa kwa Sh1.26 bilioni lililopo Mapinga, katika Manispaa ya Kinondoni lenye ukubwa wa hekta 127, lakini ni hekta 58 tu zilizokuwa zimetengwa na kufanyiwa kazi.
Ununuaji Pan Africa Energy
Dosari nyingine katika ripoti hiyo ni mkataba wa NSSF na Yakubu and Associates Chambers uliosainiwa Februari 12, 2016 kwa lengo la kutoa huduma ya ushauri ili kuwezesha kupatikana kwa mshirika Kampuni ya Pan Africa Energy Limited kwa ada ya utaalamu ya Sh551.61 milioni kwa ajili ya matumizi ya ziada na kodi za ndani.
Ripoti hiyo inaeleza mshauri huyo hakuwa na uzoefu uliohitajika kama ilivyoelekezwa kwenye hadidu za rejea iliyohitaji uzoefu wa mali zisizohamishika za ndani na mambo ya mazingira, ushauri wa kodi za ndani na nje na leseni na kanuni za mfumo wa hydrocarbon.
Pia, iligundulika kuwa Kampuni ya Yakubu and Associates Chamber ndiyo iliyokuwa imesajaliwa mwaka huohuo wa kukaribisha zabuni na hivyo washauri hawakuwa na uzoefu na mazingira ya ndani.
Mshauri alitakiwa kukagua taarifa ya uchunguzi iliyoandaliwa chini ya mkataba namba NSSF/CS/20/2014-2015 ulioingiwa Desemba 11, 2014 kwa ajili ya kutoa huduma ya ushauri katika ununuzi wa Kampuni ya Pan Africa Energy Limited.
Kanuni iliyotumika ambayo ni namba 257(2)(a) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma ya mwaka 2013 (PPR, 2013), haikuwa sahihi.
Mkataba ulikuwa umeisha muda wake tangu Aprili 26, 2016, lakini uliongezwa muda kupitia kanuni namba 111(1) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma ya mwaka 2013 (PPR, 2013) inayomruhusu ofisa masuuli kuongeza muda wa mkataba na kuelezea sababu ya kufanya hivyo.
Ripoti ya CAG inasema mshauri aliwasilisha bili namba 01031604 ya Machi 1, 2016, lakini mpaka kufikia Oktoba 7, 2016 malipo yalikuwa hayajafanyika.
Kutokana na kasoro hizo, CAG ameeleza kuwa NSSF haikufuata vigezo vya kuchagua mshauri kama vilivyoainishwa kwenye Kanuni za Manunuzi ya Umma na Hadidu za Rejea (ToR) zilizoandaliwa na Bodi ya Wadhamini.
Pia, ameishauri menejimenti ya mfuko huo kuvunja au kusimamisha mkataba kwa kuwa mshauri hakuwa na uzoefu wa kutosha kufanya kazi hiyo.
Shamba la Dungu, Tuangoma
Ripoti ya CAG inaeleza kuwa NSSF iliingia mikataba yenye thamani ya Sh165.4 bilioni kwa ajili ujenzi wa kijiji cha kisasa katika shamba la Dungu na Tuangoma Kigamboni katika Manispaa ya Temeke Dar es Salaam. Mfuko ulikuwa umeshaingia gharama ya Sh73.4 bilioni.
CAG anaeleza kuwa miradi ya mfuko huo ilitekelezwa bila kufanya upembuzi yakinifu ambao ungeipa menejimenti uhakika wa uwekezaji. Kwa sababu hiyo CAG ameshindwa kupata misingi na vigezo vilivyoshawishi maamuzi ya menejimenti kuwekeza, malengo ya uwekezaji na mipango ya kurudisha fedha zilizowekezwa.
Kutokana na hali hiyo, NSSF iligundua kuwa sehemu ya ardhi ya shamba la Dungu ilikuwa inamilikiwa na Shirika la Nyumba Taifa (NHC), hivyo baadhi ya ujenzi ulihamishiwa Tuangoma.
Hata hivyo, menejimenti haikuweza kutoa nyaraka za ununuzi wa viwanja vya Tuangoma na kama vilikuwa vina ukubwa sawa, vinauzika kwenye soko na kiwango cha kurudisha uwekezaji kama ilivyo kwa Dungu.
No comments:
Post a Comment