Profesa Lipumba atinga mahakamani
Mgororo wa ruzuku ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) unazidi kupamba moto baada ya mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kwenda kuitetea mahakamani.
Profesa Lipumba na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa chama hicho, Thomas Malima wamefungua maombi Mahakama Kuu wakiomba waunganishwe kwenye kesi iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa CUF, walio upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katika kesi ya msingi ya ruzuku namba 21 ya mwaka 2017, wadai wanaiomba Mahakama imzuie msajili kutoa ruzuku kwa CUF na imuamuru Sh360 milioni alizozitoa kwa kina Profesa Lipumba zirejeshwe kwenye akaunti rasmi ya chama.
Wadaiwa katika kesi hiyo ni Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini Profesa Lipumba na Malima wamewasilisha maombi mahakamani nao waunganishwe kwenye kesi hiyo upande wa wadaiwa.
Maombi hayo yalitajwa jana na Malima aliieleza mahakama wakiwa viongozi halali wa chama hicho, wanaomba kujumuishwa kwenye shauri hilo kwa kuwa wana masilahi na shauri hilo.
Wakili wa CUF upande wa Katibu Mkuu, Juma Nassoro na Wakili wa Serikali, Hang Chang’a waliieleza mahakama kuwa bado hawajapewa hati za maombi hayo.
Jaji Wilfred Dyansobela aliamuru waombaji hao (kina Lipumba) kuwapatia nyaraka hizo na amepanga kusikiliza maombi hayo Juni 6, siku ambayo kesi ya msingi itatajwa.
No comments:
Post a Comment