Askofu Gwajima Atishwa na Matukio Ya Utekaji......Atishia Kumwanika Diamond Alivyojiunga Freemasons Kama Ataendelea Kumchokoza
Matukio ya utekaji yanayodaiwa kutokea nchini, yamemtisha Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambaye amesema Tanzania imeanza kuwa mahala pa hatari, huku akitaka vyombo vya dola vichukue hatua kuyakomesha.
Akihubiri jana katika kanisa lake lililopo Ubungo, Dar es Salaam, Gwajima aligusia tukio la kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha kwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Ben Saanane, uvamizi wa Kituo cha Televisheni cha Clouds Group na kutekwa kwa msanii wa muziki wa Hiphop, Ibrahim Mussa maarufu Roma Mkatoliki.
Katika orodha hiyo, Gwajima pia alimtaja mdogo wake, Mchungaji Samson Gwajima ambaye alidai alitekwa wiki iliyopita mkoani Mwanza.
Gwajima ambaye ibada yake hiyo ilikuwa ikirushwa mubashara na redio mtandao iliyokuwa ikisikilizwa na takribani watu 850,000 na mtandao wa Youtube uliokuwa ukifuatiliwa na watu 8,000, alilaani matukio hayo na kusema kwa sasa hata wazazi wana wasiwasi na usalama wa watoto wao, ikiwamo yeye mwenyewe ambaye wazazi wake wanamtaka aende nje ya nchi.
“Tanzania inaanza kuwa nchi ya watu kupotea kama mzuka, Ben Saanane hajaonekana hadi leo, Meneja wa Diamond alisema wa kuulizwa aliko Roma ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wakaenda akasema atapatikana kabla ya Jumapili.
“Aliyesema atapatikana Jumapili ama alijua, ana jeshi la kumfuatilia alipo, amemficha, amempa kazi maalumu ama alikuwa naye.
“Nazungumza haya kwa sababu hata mdogo wangu (Mchungaji Samson Gwajima) naye alitekwa, lakini alifanikiwa kujinasua, hivyo naunganisha watekaji wa Dar es Salaam na Mwanza,” alisema.
Alisema baadhi ya wazazi na walezi sasa wameanza kuwa na hofu na watoto wao kutokana na matukio ya utekaji yanayoendelea nchini.
Kwa mujibu wa Askofu Gwajima, wazazi wake (baba yake mzazi na baba mkwe wake), tayari wameingiwa na hofu juu ya matukio hayo.
“Ni nani anayewateka watu, anatumwa na nani, anawateka kwa manufaa gani, nani atakayefuata… mimi sitekwi ng’o, ila kama ni polisi nitakwenda.
“Tutafanya kazi saa ngapi, tutajenga nchi saa ngapi, nampenda sana Rais wangu, lakini mambo haya yanaleta picha mbaya, lazima utekaji ukome,” alisema Askofu Gwajima.
Alimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, kuchukua hatua dhidi ya matukio hayo yaliyoanza kuzoeleka nchini.
Alisema kwa hali ilivyo, waliovamia kituo cha televisheni Clouds na waliovamia studio aliyokuwamo Roma na kumchukua ni watu walewale kwa kuwa zote zilizovamiwa ni studio.
Alisema inatia shaka pale ambapo polisi wanasema mtu hayupo katika kituo chochote cha polisi, lakini baada ya muda uliotajwa na mtu asiye polisi, anayetafutwa anaibukia katika kituo cha polisi.
Gwajima alisema kwa mazingira kama hayo, inaonyesha aliyesema mtu huyo atapatikana kwenye muda huo alikuwa anajua alipo anayetafuwa, hivyo kumshauri Rais kumchukulia hatua kwa kumwondoa kwa maelezo kwamba atazidi kuiaibisha Serikali.
“Hata mimi nawaza, hivi akiondolewa ataenda wapi, lakini nishauri tu labda apelekwe hata nje ya nchi, huko mpaka arudi huku sisi tunaojua kuwa alipata zero (sifuri) tutakuwa na miaka 60 labda, na akiwa huko nje anaweza kusoma mpaka chuo kikuu, ama akasoma hata Memkwa (Elimu ya watu wazima),” alisema Gwajima.
Katika hatua nyingine, Askofu Gwajima pia alimshambulia msanii wa muziki wa Bongo flava, Naseeb Abdul, maarufu Diamond, kwa kumwimba katika wimbo wake alioutoa hivi karibuni.
Akimzungumzia Diamond kuhusu wimbo wake uliosambazwa katika mitandao ya kijamii, alisema alikuwa amejiandaa kugeuza dhahabu kuwa maji taka kwa aliyeimba wimbo na kumtaja kwa lengo la kuunga mkono wenye vyeti feki.
Alisema hata hivyo, ameamua kumsamehe Diamond kwa sababu Biblia inakataza kumshambulia mtu aliyeomba msamaha.
Juzi baada ya wimbo huo kusambaa katika mitandao ya kijamii na kuibuka taarifa kwamba jana Gwajima angezungumzia suala hilo, Diamond kwenye ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Yala, yala jamani mwenzenu nimeyatimba, chonde chonde mzee wangu Bishop (Askofu) Gwajima usinigeuze maji kesho (jana).
“Maana nakujua ukimuamulia mtu… naweza Jumapili ya kesho (jana) nikaiona chungu mwaka mzima.”
Jana katika ibada yake, Askofu Gwajima alisema alipanga kueleza kuhusu siri ya mafanikio ya mwanamuziki huyo na mambo yanayoendelea katika maisha yake, lakini aliamua kumsamehe baada ya kuombwa radhi.
“Leo (jana) nilitaka kufundisha kuhusu Freemason na kuna bwana mmoja nitampiga ana uhusiano na Freemason. Nitaeleza tarehe aliyojiunga, mahala, alimtoa nani (kafara), ofisi yake ikoje na kinachoendelea kwenye maisha yake.
“Kabla hujamwimba Mchungaji Gwajima, lazima uwaze mara mbilimbili na wimbo wako uurudie mara mbilimbili kabla hujaupiga ili ujue madhara yake… nataka kumwonyesha namfahamu na nikikuongelea utabaki vipande vipande,” alisema.
Askofu Gwajima alisema ana roho mtakatifu anayemsaidia kuwafyatua watu na akatahadharisha watu wanaojaribu kumshambulia wajue wanashambulia mdomo wa Jehova.
“Umetoa wapi ujasiri wa kusema juu ya masihi wa bwana? Ukinichokoza uwe umevaa suti ya chuma, mavazi ya kawaida nitayachana, watumishi wa Mungu unapotaka kuwachokoza tafakari mara mbilimbili,” alisema Gwajima.
Askofu Gwajima alisema amemsamehe Daiamond, lakini anampa onyo na kama akirudia tena hata akiomba msamaha hatamsamehe.
“Biblia inatuzuia kumpiga mtu aliyeomba msamaha na mimi namsamehe, lakini nampa onyo atakaposogeza pua yake tena, hata akiomba msamaha nitajua amezoea, hivyo atageuka sembe… ujumbe umeupata almasi,” alisema.
Katika ibada hiyo, pia Askofu Gwajima aliendesha maombi maalumu yaliyokuwa na lengo la kuiombea nchi iondokane na matatizo mbalimbali yakiwamo ya utekaji.
“Kama kuna kafara imetolewa watu wawe wanatekwa, tunafanya maombi maalumu juu ya nchi kwa ajili ya kuibomoa kafara hiyo,”alisema Askofu Gwajima na kushangiliwa na waumini wake.
No comments:
Post a Comment