Sakata la Richmond Laibuka Tena Bungeni.......Mwakyembe Amtuhumu Joshua Nassari Kuingia na Chupa ya Konyagi Bungeni
Iikiwa imepita miaka tisa tangu alipojiuzulu aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowasa, mzimu wake umeendelea kumtesa Dk. Harrison Mwakyembe, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge kuhusu suala la Richmond.
Hatua hiyo inatokana kuibuka kwa suala la Richmond bungeni juzi, hali iliyosababisha kutupiana vijembe kati yake na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema).
Juzi, Dk. Mwakyembe ambaye sasa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, akijibu matamshi ya Nassari, alidai mbunge huyo aliingia bungeni akiwa amelewa.
Alidai mkakati uliopo wa Chadema kumsafisha Lowassa hautafanikiwa.
Jana, akizungumza bungeni wakati wa kutihimisha mjadala wa hotuba ya makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Rais Tamisemi pamoja na ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mwakyembe, alijibu tena ‘makombora’ yaliyorushwa kwake na Nassari juzi.
“Suala la Richmond limeibuliwa jana (juzi) na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mheshimiwa Nassari kwamba Kamati Teule iliyochunguza suala hilo, haikumtendea haki Mheshimiwa Edward Lowassa kwa sababu haikumuhoji.
“Mimi naelewa ni kazi mgumu sana leo (jana) hii kutaka kumsafisha Mheshimiwa Edward Lowassa na kesi ya Richmond ilikwisha na ndiyo maana sioni ajabu kusema aliyoyasema ilibidi Nassari anywe pombe kwanza.
“Na nayasema haya kiongozi wa upinzani bungeni ajue kwamba tuna tatizo hilo na mimi nawapongeza sana vijana wetu wa usalama waliokamata hiyo chupa na angeruhusiwa na hiyo chupa huenda angeweza akatapikia hata rangi zetu za Taifa humu ndani ingekuwa ni scandal (kashfa) kubwa.
“Mheshimiwa mimi nimelezea mara nyingi sana katika Bunge hili, hata Bunge la tisa lililoshughulikia suala la Richmond kuwa Kamati Teule iliyoundwa na Bunge hili kazi yake ilikuwa kuchunguza siyo kutoa uamuzi,” alisema Dk. Mwakyembe.
Msomi huyo na mwalimu wa sheria, alisema wakati wa kufanya uchunguzi suala la kusikiliza upande mwingine halipo, upo wakati wa uamuzi na ndiyo maana kamati yake iliwasilisha ripoti bungeni ikiwa na mashahidi 40 nje ya Bunge.
“Aliyetakiwa kuhojiwa hapa akajiuzulu, unamlaumu Mwakyembe kwa hilo? Naomba msipotoshe umma kuwa hakuhojiwa, ahojiwe vipi?
“Unajua ni aibu, ni sawa na mtu anaenda mahakamani anasema unajua polisi hawakunipa haki ya kuhojiwa….polisi? Uko mahakamani ndiyo pa kukuhojiwa hapo,” alisema.
Alisema kamati yake ilikuwa na nyaraka za Serikali 104 na iliwahoji watu 75 ambao waliulizwa maswali 2,717.
Dk. Mwakyembe alisema, kwa sababu hiyo kamati yake haikuona sababu yoyote ya kumuhoji Lowassa kwa sababu ilikuwa na kila kitu.
“Mimi niombe Mheshimiwa mwenyekiti, kama kuna mtu yeyote hapa bado anakereketwa na kesi ya Richmond, aache maneno maneno hapa, leta hiyo kesi hapa kama hatujawanyoa nywele kwa kipande cha chupa.
“Ileta hapa, acha maneno ya kienyeji hapa, tumeshachoka, jamani hee…ileteni hiyo kesi hapa, mnaruhusiwa na kanuni.
“Naomba nimalizie kwamba, mimi naahidi, siku ambayo kuna mmoja atakuwa jasiri wa kusema analeta suala la Richmond hapa, mimi naahidi nitamuomba Mheshimiwa Rais anipumzishe uwaziri niweze kuishughulikia hiyo kesi kwa ukamilifu iishe moja kwa moja.
“Mheshimiwa Mwenyekiti kuna hoja nyingine ambayo aliieleza kwenye andiko langu la Shahada ya Uzamivu niliandika kuhusu Serikali tatu lakini hivi sasa nasema kuhusu Serikali mbili,” alisema Dk. Mwakyembe.
Akizungumza matamshi ya Nassari juzi kuwa hiyo inaonyesha jinsi Waziri huyo alivyo kigeugeukwa kuandika kuwa ili Tanzania iende mbele inahitaji serikali tatu, lakini akageuka wakati wa Bunge Maalumu la Katiba na kuunga mkono serikali mbili, Mwakyembe alisema: “Alilewa (Nassari), ndiyo maana alikuwa anasema tu, alikuwa ameambiwa, hajasoma hata hilo andiko,” na kuongeza:
“Na hapa ndiyo unaelewa watu wasio na integrity, unawajua hapa. Ambao wanakesha miaka mitano kumtukana mtu kwa kumwita fisadi, leo wanamkumbatia wanalamba na nyayo zake, ndiyo vigeugeu namba moja hao”.
Hata hivyo, kabla hajamaliza kuzungumza alisimama Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) na kuomba mwongozo na utaratibu kwa mujibu wa Kanuni ya 64(1).
Alisema: “Kwa mujibu wa Hansard za Bunge, Dk. Mwakyembe alisema Mheshimiwa Edward Lowassa alijiuzulu kwa mambo yaliyofanywa na walio chini yake, leo (jana) Dk. Mwakyembe anasema ana ushahidi wa asilimia 100 kwamba Lowassa alihusika 100 kwa 100 na jambo hilo.
“Naomba kwa idhini yako unipe muda niwasilishe Hansard hapa kwenye Bunge hili kuthibitisha maneno ya Dk. Mwakyembe ya Februari mwaka 2008”.
Kubenea alisema jambo la pili ni kuhusu tuhuma za Dk. Mwakyembe kwamba juzi Nassari alikuwa na chupa ya Konyagi na aliingia nayo bungeni.
“Siyo kweli, nina uwezo wa kulithibitishia Bunge hili kwamba Nassari jana hakuwa amelewa. Tulikuwa naye mchana kutwa na alikuwa amekuja bungeni na soda ambayo ilikuwa imewekwa kwenye chupa,”alisema.
Baada ya maelezo hayo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alisema kwa taarifa alizo nazo, chupa anayodaiwa kuwa nayo Nassari ilikuwa ni nje ya Bunge wala siyo ndani ya Bunge kama inavyodaiwa.
Nje ya Ukumbi wa Bunge, Nassari alisema alijibu tuhuma hizo za Dk. Mwakyembe kwa sababu kitendo cha Serikali kuhangaika naye tangu juzi ni kwamba amewagusa sehemu nyeti na Waziri huyo (Dk. Mwakyembe) si mtu wa kuaminika.
No comments:
Post a Comment