Serikali kudhibiti biashara ya vyuma chakavu
Na Daudi Manongi-MAELEZO, DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeandaa Rasimu ya Muswada wa Sheria itakayoweka bayana taratibu na mfumo wa usimamizi na udhibiti wa bishara ya chuma chakavu katika hatua mbalimbali za uzalishaji, ukusanyaji, usambazaji, uuzaji na uyeyushaji wake kwa kuzingatia uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa manufaa ya Taifa.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge Mjini Dodoma.
"Biashara ya Chuma chakavu imeshamiri hapa nchini na duniani kwa ujumla na hili limetokana na mahitaji ya vyuma chakavu ambapo kumetumiwa na wahalifu kuharibu miundombinu iliyojengwa kwa vyuma kwa nia ya kupata chuma ili waiuze kama chuma chakavu"Alisema Mwijage.
Alisema ili kukabiliana na hujuma hizi Mamlaka husika zikiwemo TANESCO, TANROADS na RAHCO wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na jeshi la Polisi ikiwemo kutumia walinzi wa Taasisi husika ili kulinda rasilimali hizo.
Alisisitiza kuwa Muswada huu umeweka wazi na bayana adhabu itakayotolewa kwa mtu atakayebainika kuharibu miundombinu.
Aidha Mhe.Mwijage alitoa wito kwa watanzania kutoa taarifa pindi waonapo mtu anayehujumu miundombinu kwa namna yote ile.
“Natoa wito kwa wenye viwanda na wafanyabiashara wa vyuma chakavu jiepusheni na ununuzi wa vyuma ambavyo asili yake ina mashaka na tutaharakisha sheria hii ili kutatua tatizo hili,” aliongeza Mwijage.
No comments:
Post a Comment