Lowassa Atema Cheche Arusha Akimnadi Mgombea Udiwani wa CHADEMA
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema mabadiliko makubwa ya kisiasa yanayotokea duniani katika kipindi hiki hayawezi kuzuiliwa na mifumo iliyopo.
Akizungumza jana na mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Mateves katika Halmashauri ya Arusha Vijijini, Lowassa alisema nguvu kubwa ya mabadiliko inayoonyeshwa na Chadema itawaletea wananchi maendeleo.
Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, chama chake kilipata kura nyingi kwenye maeneo mengi licha ya kutokuwa washindi na kwamba wamejipanga katika uchaguzi wowote utakaofanyika kuhakikisha kinashinda kwa kishindo.
“Ninazindua kampeni za uchaguzi huu mdogo nikiwa na imani kubwa kwa Chadema. Nina imani kuwa mgombea wa chama hiki atatekeleza anayoyaahidi na kuondoa kero zenu na ndiyo maana Chadema inaungwa mkono zaidi nchini,” alisema Lowassa.
Alisema katika mpango wa kukiimarisha chama hicho, wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wanazunguka nchi nzima kuanzia ngazi ya tawi hadi Taifa.
Katika harakati za kuhakikisha kwamba upinzani unaibuka na ushindi katika chaguzi ndogo zote zilizopangwa kufanyika Januari 22, Lowassa alisema leo atakuwa Zanzibar katika uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhan na baada ya hapo ataelekea Bukoba katika kampeni za Ukawa.
Uchaguzi wa Kata ya Mateves unafanyika baada ya Mahakama kuagiza urudiwe kutokana na kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi ulipita ambao mgombea wa CCM alitangazwa mshindi.
No comments:
Post a Comment