Nyota wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samata amesema kwamba anaimani na Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo, Salum Mayanga kwamba anaweza kuiletea mafanikio.
Mshambuliaji huyo wa KRC Genk, amesema kwamba Mayanga ni kocha mwenye uzoefu kwa sasa na anawajua wachezaji wa Tanzania, hivyo anaweza kufanikiwa.
Samatta aliyewasili usiku wa juzi kujiunga na kikosi cha Stars kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki za kimataifa wiki ijayo dhidi ya Botswana Jumamosi na Burundi Jumanne, amesifu pia uteuzi wa kikosi cha Stars wa Mayanga, kwamba umezingatia makosa yaliyojitokeza kwa walimu waliomtangulia.
Alipoulizwa na waandishi kuhusu mtazamo wake juu ya Mayanga, Samata alisema "Alikuwa kocha msaidizi kipindi cha Mart Noij na tulikuwa tunafanya kazi pamoja kwenye timu ya taifa tunafahamia na anawafahamu wachezaji wengi wa kitanzania wa timu ya taifa."
Tayari Mayanga amewateua viungo Himid Mao Mkami wa Azam FC na Jonas Gerald Mkude wa Simba, kuwa Manahodha wasaidizi wa timu hiyo, kufuatia aliyekuwa Nahodha Msaidizi na Nahodha wa kikosi cha wachezaji wa nyumbani, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ kuwa majeruhi tangu Januari mwaka huu.
Taifa Stars inatarajiwa kucheza mechi mbili, kwanza na Botswana Machi 25 na baadaye Burundi Machi 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na pamoja na Samatta, mchezaji mwingine wa Tanzania anayecheza Ulaya, Farid Mussa wa Tenerife ya Hispania anatarajiwa pia kuwasili kesho.
No comments:
Post a Comment