Sophia Simba: Sina Mpango wa Kuiunga na Chama Chochote cha Upinzani
Aliyekuwa mwanachama mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba ambaye alifukuzwa uanachama kwa usaliti, amezungumzia hatua aliyoichukua baada ya uamuzi huo dhidi yake.
Wikendi iliyopita, CCM ilitangaza kumvua uanachama Mwanasiasa huyo baada ya kumtia hatiani, ambapo taarifa zinadai kuwa yeye alibainika kwenda nyumbani kwa aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa hata baada ya uchaguzi mkuu akiwa amevalia hijabu kujificha. Hali iliyotafsiriwa kuwa alikuwa akimpelekea siri za chama.
Baada ya uamuzi huo wa CCM kutangazwa, Lowassa alimkaribisha Sophia Simba na wenzake 12 waliofukuzwa, kujiunga na Chadema huku akiwaita mashujaa waliokuwa wanatetea demokrasia ndani ya chama hicho tawala.
Hata hivyo, Sophia Simba amesema kuwa hana mpango na hatahamia katika chama chochote kwani maisha yake yote yametokana na kuitumikia CCM.
Mwanasiasa huyo ambaye alijiunga na CCM tangu ilipozaliwa mwaka 1977 na kushika nyadhifa mbalimbali baadae, amesema kuwa atabaki kuwa mkereketwa wa chama hicho.
“Napenda kuwaeleza Watanzania wote, wafahamu kuwa sina mpango wowote wa kujiunga na upinzani. Na unajua CCM ina makundi mawili, la kwanza ni wanachama wenye kadi na la pili wakereketwa ambao ni wengi. Na mimi nitaingia katika kundi hilo na sio kuhama,” Sophia Simba anakaririwa na Mtanzania.
Aidha, alikanusha taarifa zilizokuwa zimeripotiwa kwenye baadhi ya mitandao kuwa amekutana na mwanasiasa mmoja wa upinzani. Alisisitiza kuwa hakufanya hivyo na hana mpango huo.
Akizungumzia tuhuma za kukisaliti chama hicho zilizopelekea kung’olewa kwake, alikana kuwa msaliti wa chama hicho ingawa alisisitiza kuwa hataki kulizungumzia kwa undani bali anamuachia Mungu anayeiona nafsi yake.
“Sitaki kuzungumzia kwa udani suala la usaliti ila kwa ufupi, Mungu anaishuhudia nafsi yangu. Jamani, hivi kweli nikisaliti chama changu ambacho kimenilea katika maisha yangu yote!”
Katika hatua nyingine, alisema kuwa hana mpango wa kwenda mahakamani kutafuta haki ya kurejea ndani ya chama hicho kwani kufanya hivyo ni kukosa fadhila kwa jinsi ambavyo chama hicho kimempa maisha.
Mwanasiasa huyo mkongwe alisema kuwa amepokea adhabu aliyopewa kwa mikono miwili na kwamba hana kinyongo.
No comments:
Post a Comment