Dr. Makongoro Mahanga Atoweka.....Polisi Waendelea Kumsaka
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk. Makongoro Mahanga, anayesakwa na Jeshi la Polisi ametoweka nyumbani kwake.
Mahanga anasakwa na polisi kutokana na amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyoamuru akamatwe kwa kushindwa kumlipa Kainerugaba Msemakweli zaidi ya Sh milioni 11 za kesi ya madai aliyomshinda.
Mahakama hiyo ilitoa amri ya kukamatwa Machi 7, mwaka huu na kutoa nyingine mwishoni mwaka wiki ambapo alitakiwa kufikishwa mahakamani jana. Hata hivyo hakupatikana.
“Makongoro Mahanga hajaja mahakamani na nyumbani kwake hayupo, anaendelea kutafutwa,” alisema Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu, Ruth Masambu.
Hadi jana, Mahakama Kuu ilishatoa hati mbili kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala, ikielekeza Mahanga akamatwe na kufikishwa mahakamani.
Msemakweli ambaye ni mlalamikaji, alikabidhiwa hati hiyo na kutakiwa kumkabidhi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, ili aweze kutekeleza amri hiyo.
Hamduni alikiri kupokea hati hiyo na kusema mdaiwa hajapatikana hivyo wanaendelea kumtafuta.
Dk. Mahanga, anatakiwa kumlipa mwanaharakati huyo baada ya kesi aliyofungua ya kashfa dhidi yake kufutwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment