CUF ya Maalim Seif kuiburuza CUF ya Prof.Lipumba mahakamani
Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF ), imefungua kesi ya madai dhidi ya wanachama wake nane akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya
Kesi hiyo imefunguliwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikitaka wanachama hao wasijihusishe na harakati zozote za chama hicho.
Mbali ya Sakaya ambaye pia ni mbunge wa Kaliua mkoani Tabora, wadaiwa wengine ni Thomas Malima, mbunge wa Mtwara Mjini,Mafta Nachumu, Omar Mhina Masoud, Abdul Kambaya, Salama Masoud, Zainabu Mndolwa na Jafari Mneke.
Maombi hayo mbayo yametajwa mbele ya Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri yamewasilishwa na Wakili wa bodi, Hashim Mziray na yamepangwa kusikilizwa kesho.
Katika maombi hayo yaliyopewa namba 1 ya mwaka 2017, bodi inaiomba mahakama kutoa zuio kwa wadaiwa kutojihusisha katika masuala yeyote yanayohusiana na chama hicho.
Mbali ya maombi hayo, pia Wakili Mziray amewasilisha maombi madogo ya kuiomba mahakama kuwaamuru wadaiwa wasijihusishe na mikutano ya chama hicho.
Aidha, Mziray aliomba maombi yao madogo yasikilizwe kwa upande mmoja wa wadai tu kwa kuwa wamechelewa kuwapatia nyaraka za madai yao wadaiwa.
"Mheshimiwa tunaomba tusikilizwe upande mmoja ukizingatia maombi yameletwa chini ya hati ya dharula na kwa mujibu wa sheria mahakama hii... inayo mamlaka ya kufanya hivyo".
Hakimu Mashauri alisema anakubaliana na upande wa wadai na maombi hayo yatasikilizwa kesho mahakamani hapo.
Hatua ya Bodi ya CUF, kukimbilia mahakamani inakuja ikiwa ni siku moja baada ya upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hammad kupinga uteuzi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Uteuzi wa Profesa Lipumba ambao unapingwa ni ule alioufanya Machi 6, mwaka huu baada kuwaondoa katika nafasi zao, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Omar Ali Shehe.
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Salim Abdull Bimani, Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, Abdullah Bakar Hassan.
Wengine ni Pavu Juma, Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadam na Sheria, Mahmoud Ali Mahindo na Katibu wa Jumuiya ya Vijana, Yusuph Salim.
No comments:
Post a Comment