Mrisho Ngasa alikataa Goli la Ibrahim Ajib
Kiungo mshambuliaji wa Mbeya City, Mrisho Ngassa, ameweka wazi kuwa bao alilofunga kiungo wa Simba, Ibrahim Ajibu siyo la halali kutokana na mazingira ya lilivyopatikana ambapo anaamini haikuwa faulo kama maamuzi ya mwamuzi yalivyokuwa.
Ngassa alikuwa sehemu ya kikosi cha Mbeya City ambacho kilitoka sare ya mabao 2-2 na Simba kwenye mchezo wa ligi kuu ambao ulipigwa Uwanja wa Taifa, Dar. Mabao ya Mbeya City yalifungwa na Ditram Nchimbi na Kenny Ally wakati yale ya Simba yalifungwa na Ibrahim Ajibu na Shiza Kichuya kwa penalti.
Ngassa ambaye amewahi kuzichezea Yanga, Azam na Simba kwa nyakati tofauti, amesema kwamba bao hilo la Ajibu halikuwa halali kwa sababu hakukuwa na faulo yoyote ambayo ilifanywa na mabeki wa timu hiyo kwa kiungo Mohammed Ibrahim ‘Cabaye’.
“Lile bao la Ajibu siyo halali kwa sababu hatukufanya faulo yoyote kama mwamuzi alivyodai kwa sababu beki wetu alizuia mpira na siyo kumchezea rafu Mohammed Ibrahim ambaye alianguka na mwamuzi akaruhusu kupigwa faulo hiyo ambayo iliipa Simba bao.
“Lakini bao la pili ambalo walilipata kwa penalti wala sina shaka nalo kwa sababu mchezaji wao alifanyiwa faulo kweli kwenye eneo la hatari ambalo lazima pigo hilo litolewe.
“Lakini kiukweli mechi ilikuwa nzuri na kila timu ilikuwa na nafasi ya kushinda lakini mwisho ndiyo matokeo hayo yametokea lakini tunaenda kujipanga kwa ajili ya mechi zinazokuja ambazo naamini tutafanya vizuri,” alisema Ngassa ambaye ametokea Fanja ya Oman kabla ya kutua Mbeya City.
No comments:
Post a Comment