CUF Yanyimwa Ruzuku....Maalim Seif Ataja Hujuma 9 Zinazofanywa na Profesa Lipumba
Katibu
Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ameibuka na kutaja utatu
unaojumuisha mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, Msajili
wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Jeshi la Polisi akieleza
ndio unaoshirikiana kukihujumu chama hicho, huku akibainisha mambo tisa
anayoeleza kuwa ‘ushahidi wa ushirikiano’ na hujuma hizo.
Akizungumza
katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuibuka kwa mgogoro ndani ya
chama hicho baada ya Jaji Mutungi kumtambua profesa Lipumba kuwa
mwenyekiti wa CUF, Maalim Seif alitumia dakika 95 kueleza hujuma hizo na
kudai zinalenga kukifanya chama hicho kutodai haki ya kunyang’anywa
ushindi wa Uchaguzi Mkuu Zanzibar.
Akiwa
sambamba na viongozi mbalimbali wa chama hicho, alisema hana ugomvi na
Profesa Lipumba na yupo tayari kukaa naye meza moja kueleza uongo wa
mtaalamu huyo wa uchumi, ikiwa ni pamoja na ukweli anaouficha kuhusu
kujiuzulu kwake uenyekiti wa CUF Agosti mwaka jana na uamuzi wake wa
kutaka kurejea katika chama hicho.
Mbali
na kukiri CUF kupitia katika wakati mgumu kwa sasa, Maalim Seif alisema
hujuma hizo zilizotokana na ‘wakubwa’ kuchukizwa na kitendo cha chama
hicho kuwasilisha vielelezo Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC)
vinavyowatuhumu viongozi wa Serikali kutumia mamlaka yao vibaya katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, zimesababisha chama hicho kutopata ruzuku
ya Sh milioni 117 kila mwezi, tangu Agosti mwaka huu.
“Mtiririko
wa matukio haya (tisa) yanaonesha wazi hujuma hizi…, ni mambo
yanayoratibiwa kwa suhirikiano wa makusudi kati ya msajili, polisi na
Lipumba, “ alisema Maalim Seif.
Aliyataja
mambo hayo kuwa ni kuvamiwa kwa Mkutano Mkuu wa CUF iliofanyika Agosti
21, utekaji wa wanachama na viongozi wa chama hicho, kuvamiwa kwa ofisi
kuu iliyopo Buguruni, kuvunjwa kwa ofisi za wilaya ya Bagamoyo na
Mkuranga, wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho
kuzuiwa kufanya kikao cha ndani.
Mengine
ni kuzuiwa kufanyika kwa mkutano mkuu maalumu wilaya ya Tanga, utekaji
wa mlinzi wa chama hicho uliofanyika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, kuzuiwa kwa kikao cha ndani mkoani Mtwara pamoja na walinzi wa
Profesa Lipumba kutaka kuzuia viongozi wa CUF kuingia chumba cha
mahakama kuu hiyo.
Agosti
8 mwaka jana Profesa Lipumba alitangaza kuachana na uongozi wa chama
hicho, baada ya CUF kukubaliana na Ukawa kumsimamisha Edward Lowassa
kuwania urais.
Hata
hivyo, Juni mwaka huu Profesa huyo aliomba kwa barua kurejea kwenye
wadhifa wake, ambao kwa sasa unashikiliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro aliyechaguliwa katika mkutano wa Baraza
Kuu la Uongozi la chama hicho.
Uamuzi
wake huo ulizua sintofahamu ndani ya CUF huku mkutano mkuu wa dharura
wa chama hicho uliofanyika Agosti 21 mwaka huu kumchagua mwenyekiti
mpya ukivunjika baada ya kundi la wafuasi wa chama hicho kuvamia na
kufanikiwa kuzima mchakato wa kupiga kura kumchagua mwenyekiti mpya,
wakishinikiza Profesa Lipumba aruhusiwe kurejea katika wadhifa huo.
Baada
ya sakata hilo Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho lilimvua uanachama
Profesa Lipumba na kuwasimamisha uanachama makada kadhaa wa CUF, jambo
ambalo liliingiliwa kati na Msajili wa Vyama vya Siasa aliyetoa waraka
wa kumtambua Lipumba kuwa mwenyekiti.
Kitendo
cha Lipumba kutambuliwa na kurejea katika chama hicho kilisababisha
Baraza la Wadhamini la CUF kufungua kesi Mahakama Kuu na kumshtaki
profesa huyo Jaji Mutungi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George
Masaju.
Katika
ufafanuzi wake, Maalim Seif alisema Lipumba alivamia Mkutano Mkuu wa
chama hicho akiongozwa na polisi na kusababisha vurugu kubwa sambamba na
uharibifu wa mali lakini polisi haikuchukua hatua yoyote.
“Kumekuwa
na matukio kadha aya utekaji wa viongozi na wanachama wa CUF…,
mkurugenzi wetu wa fedha Joram Bashange alitekwa akiwa anatoka nyumbani
kwake na walinzi wa Lipumba, licha ya kukamatwa na kufikishwa polisi
waliachiwa na gari walilotumia nalo halipo kituo cha polisi buguruni,” alisema.
Alisema
Septemba 24 mwaka huu, Lipumba na wafuasi wake walivamia ofisi kuu ya
CUF iliyopo Buguruni na kufanya uharibifu huku akipewa ulinzi mkali wa
polisi.
“Polisi
kazi yao ni ulinzi wa raia na mali zao pamoja na kupambana na wahalifu
lakini hivi sasa wao ndio wanatetea wahalifu. Tunamuomba Mwigulu
(Nchemba-Waziri wa Mambo ya Ndani) kuingilia kati na kutizama watendaji
walio chini ya wizara yake,” alisema Maalim Seif.
Alisema
tukio la nne ambalo polisi imeshindwa kukamata wahusika licha ya
kuwajua ni uvamizi uliofanywa na wafuasi wa Lipumba wa kuvunja ofisi za
chama hicho wilayani Bagamoyo na Mkuranga.
“Wabunge
na wajumbe wa Baraza Kuu la uongozi la chama walizuiwa kufanya kikao
cha ndani Newala na kukamatwa walipokuwa Nachingwea,” alisema na kubainisha kuwa wakati viongozi hao wakikamatwa, Lipumba anafanya vikao kama hivyo bila kukamatwa.
“Polisi
walizuia kufanyika kwa mkutano mkuu maalum wa wilaya ya Tanga kwa madai
kuna pande mbili zinavutana. Pia Novemba 10 mwaka huu mlinzi wa chama,
Mohamed Said alitekwa akiwa mahakama kuu na kupigwa sana na
kunyang’anywa fedha na kupelekwa kuhojiwa na Lipumba. Tukio hilo
lilitokea mbele ya polisi,” alisema.
Alisema
jeshi hilo pia lilizuia kufanyika kwa kikao cha ndani mkoani Mtwara
pamoja na walinzi wa Lipumba kutaka kuzuia viongozi wa CUF kuingia ndani
ya chumba cha mahakama kufuatilia shauri lao, huku akimtaja mmoja wa
walinzi hao kuwa ni Hassan Kingwele.
Akijibu
hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Lipumba, Maalim alisema msomi huyo
anatumiwa na dola na kubainisha kuwa anaficha ukweli juu ya uamuzi wake
wa kujiondoa CUF.
“Lipumba
bado hajasema sababu za kweli juu ya kujiuzulu kwake, yeye ndio alikuwa
mwanzilishi wa Ukawa katika Bunge Maalum la Katiba na ndio aliyemtafuta
Lowassa na kumshawishi awanie urais kupitia Ukawa,” alisema.
“Lowassa
ilikuwa ajiunge na NCCR kwa sababu ni chama kidogo ili CUF na Chadema
tumuunge mkono kwa mantiki hiyo iweje Lipumba aseme mimi sikumshirikisha
ujio wa Lowassa ndani ya Ukawa?”
Alisema
yeye hana ugomvi na Lipumba bali mtaalam huyo wa uchumi ana ugomvi na
CUF, huku akidai kuwa hivi sasa anatumia udini, ukabila na uzanzibari
kukigawa chama hicho.
“Hizi ni jitihada za dola kunifanya nisidai haki kwa yaliyotokea Zanzibar…, hilo halitawezekana nitaidai tu mpaka mwisho,” alisema.
No comments:
Post a Comment