Trump: Nigel Farage atakuwa balozi bora wa Uingereza
Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema kiongozi wa mpito wa UKIP Nigel Farage angekuwa balozi mzuri sana wa kuiwakilisha Uingereza nchini Marekani.
Bw Trump aliandika kwenye Twitter kwamba 'watu wengi' wangependa kumuona Bw Farage kama balozi na atafanya kazi 'njema'.
Bw Farage aliyemuunga mkono Bw Trump wakati wa kampeni za uchanguzi amesema tamko hilo hakulitarajia. Hata hivyo aliongezea: ''iwapo ningekuwa na uwezo wa kuisaidia Uingereza kwa njia yoyote ile ningeisaidia''.
Bw Farage ambaye ni kaimu kuongozi wa UKIP, alikuwa mwanasiasa wa kwanza Mwingereza kukutana na Trump baada ya ushindi wake, na kusema kuna ''nafasi bora'' ya kuimarisha biashara ya Uingereza na Marekani.
Alisema: ''Ni jambo la kushangaza kwangu. Hakuna aliyekuwa amenidokezea kuhusu swala hio lakini nina uhusiano mwema na watu wake na iwapo nitaweza kuisaidia Uingereza kwa njia yoyote ile, niko radhi kuisaidia."
Bwana Trump ni ''mtu anayeipenda Uingereza kwa dhati na rafiki wa jamii wa nchi yake,''Bw Farage aliongeza
Bw Trump alizungumza na Waziri Mkuu wa Uingereza Bi Theresa May kwa njia ya simu na kumeshuhudiwa mawasiliano mengine kati ya mawaziri wa Uingereza na maafisa wanaoatarajiwa kuwa kwenye serikali ya Bw Trump.
Afisi ya waziri mkuu wa Uingereza, ikijibu tamko la Bw Trump, imesema "hakuna nafasi ya kazi iliyo wazi. Tuna balozi mzuri Marekani."
Mhariri msimamizi wa maswala ya kisiasa wa BBC Norman Smith, anasema afisi ya waziri mkuu wa Uingereza inaonekana kusisitiza kwamba hakutakuwa na nafasi yoyote ya kazi kwa Bw Farage.
Kiongozi wa Liberal Democrat, Tim Farron alichapisha kwenye mtandao wa Twitter, ujumbe kwamba pendekezo la kumtuma Farage kama balozi wa Uingereza kwa Marekani , ''ni hatua ya kijinga''.
Aliongeza: "Sina diplomasia kwa vidole vyangu hivi vidogo. Lakini kitu kinachonishangaza ni (mpango wa Bw Trump) kujiondoa kwa mkataba wa kibiashara wa Pasifiki (TPP)."
Bw Farron alikuwa akizungumzia tangazo la Bw Trump la kuwa ataiondoa Marekani kutoka kwenye mkataba huo siku yake ya kwanza akihudumu kama rais.
No comments:
Post a Comment