Donald Trump asema Fidel Castro alikuwa ‘dikteta katili’
Rais Mteule wa Marekani Donald Trump amesema kiongozi wa zamani wa Cuba Fidel Castro alikuwa "dikteta katili" saa chache baada ya Bw Castro kufariki dunia akiwa na miaka 90.
Bw Trump amesema: "Leo, ulimwengu umeshuhudia kifo cha dikteta katili aliyewakandamiza watu wake kwa karibu miongo sita. Utawala wake ulikuwa wa watu kuuawa kwa kupigwa risasi, wizi, mateso yasiyoweza kufikirika, umaskini na ukiukaji wa haki za kibinadamu.
"Ingawa Cuba inasalia kuwa kisiwa chini ya utawala wa kiimla, matumaini yangu ni kwamba siku ya leo ni mwanzo wa kuondokea mambo ya kuogofya ambayo yamevumiliwa kwa muda mrefu, na kuelekea siku za usoni ambapo watu wazuri wa Cuba hatimaye wataishi kwa uhuru ambao wanastahili sana.
"Ingawa mikasa, vigo na uchungu uliosababishwa an Fidel Castro haviwezi kufutwa, utawala wetu utajaribu kadiri uwezavyo kuhakikisha watu wa Cuba hatimaye wanaweza kuanza safari yao ya kuelekea kwa ufanisi na uhuru.
Najiunga na Wamarekani wengi kutoka Cuba ambao waliniunga mkono sana katika kampeni yangu ya urais, wakiwemo chama cha maveterani wa Brigade 2506 ambacho kiliniidhinisha, kwa matumaini kwamba siku moja hivi karibuni tutapata Cuba huru."
Rais Barack Obama, ambaye chini yake Marekani ilirejesha uhusiano wa kidiplomasia na Havana baada ya miongo mingi ya uhasama, alisema historia "itanakili na kuwa mwamuzi wa mchango muhimu" wa Castro.
Alisema Marekani imefanya kazi kwa bidii kuweka nyuma yaliyopita kati yetu na kunyoosha "mkono wa urafiki kwa watu wa Cuba" kwa wakati huu.
No comments:
Post a Comment