Kauli ya Jeshi la Polisi Kuhusu Askari wake Aliyefariki Dunia Kwa Kujipiga Risasi
Jeshi la Polisi mkoani Pwani limezungumzia kifo cha askari wake PC Armand Furaha (33) aliyejipiga risasi kifuani bila kukusudia na kufariki dunia.
Askari huyo alijipiga risasi hiyo usiku akiwa anaelekea kwenye lindo nyumbani kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha.
Tulio hilo lilitokea saa moja usiku eneo la Mailimoja sokoni usiku wa kuamkia jana, wakati askari huyo akiwa njiani kuelekea kwenye kituo cha lindo alichopangiwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Pwani, Blasius Chatanda amesema askari huyo alijipiga risasi bahati mbaya kwa bunduki aina ya SMG akiwa amekaa kwenye kiti cha mbele katika gari alilokuwa anasafiria kwenda lindoni.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa askari huyo alikuwa tayari ameweka risasi chemba kwenye bunduki hiyo aliyokuwa nayo na kwa bahati mbaya akiwa anashuka kwenye hilo gari ndipo risasi hiyo ikafyatuka na kumpiga kifuani eneo la kushoto na kufa wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Tumbi.
“Kabla ya tukio hilo, askari huyu aliwasili kazini jioni na kukuta amepangiwa kituo cha ulinzi kwa mkuu wa wilaya hivyo kama ilivyo ada alichukua zana za kazi ikiwemo bunduki hiyo na kuanza safari ya kuelekea lindoni kwake huko kwa DC, lakini bahati mbaya hakufika alifariki kwa kujipiga risasi bahati mbaya,” amesema Chatanda.
Akizungumzia suala la askari kujipiga risasi Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba amesema kila tukio hutokana na mazingira tofauti.
No comments:
Post a Comment