Rais Magufuli afanya mazungumzo na Rais Mstaafu Mwinyi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 23 Novemba, 2016 amekutana na kufanya Mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaji Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo, Alhaji Dkt. Ali Hassan Mwinyi amesema lengo la kukutana na Rais Magufuli na kufanya nae mazungumzo kwa mara ya kwanza ni kumpongeza kwa kutimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani na pia kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake.
Alhaji Dkt. Ali Hassan Mwinyi ameyataja baadhi ya maeneo ambayo Rais Magufuli ameyafanya kwa mafanikio makubwa kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa na amebainisha kuwa hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha mwaka mmoja zimedhihirisha kasi kubwa ya kukabiliana na tatizo hilo ikilinganishwa na wakati uliopita.
“Rushwa ilikuwepo tangu enzi ya Hayati Mwalimu Nyerere, aliipondaponda kabisa lakini hakuimaliza, na sote tuliosalia ni hivyo hivyo, kila mmoja amefanya kwa kiasi chake, lakini Rais Magufuli kwa mwaka mmoja ameleta Sunami, nafurahi sana” amesema Alhaji Mwinyi.
Eneo jingine ni kuimarisha utendaji kazi Serikalini ambapo Alhaji Dkt. Ali Hassan Mwinyi amesema hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Rais Magufuli zimeongeza kasi zaidi na ametoa wito kwa Viongozi na Wananchi kuunga mkono juhudi hizo.
“Tuliobaki tumsaidie, tumsaidie kwa kumuombea Dua, tumsaidie kurekebisha kwa kusema ukweli pale ambapo watu wanapotosha, tuseme sio hivyo, ilivyo ni kadhaa kadhaa kadhaa, tusiwaache watu wakapata nafasi ya kuongea uongo, kila mtu anaweza kuwa anasema kutokana na nia yake na lengo lake, lakini hakuna asiyejua kuwa kazi aliyoifanya mwenzetu ni nzuri nzuri nzuri ya ajabu” amesisitiza Rais Mstaafu Mwinyi.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Vangimembe Lukuvi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Novemba, 2016
No comments:
Post a Comment