Tetemeko lasababisha kimbunga Fukushima, Japan
Tetemeko la ardhi la nguvu ya 7.4 kwenye vipimo vya Richter limekumba maeneo ya Fukushima na Miyagi nchini Japan na kusababisha kimbunga chenye mawimbi ya urefu wa zaidi ya mita moja.
Tetemeko hilo limetokea mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi saa za Japan (21:00 GMT Jumatatu), idara ya utabiri wa hali ya hewa ya Japan (JMA) imesema.
Wakazi walishauriwa kukimbilia maeneo yaliyo juu upesi, huku mawimbi yakihofiwa kufikia urefu wa mita 3.
Kulikuwa na taarifa za watu kadha kupata majeraha madogo pamoja na uharibifu kutokea.
Tetemeko jingine lilitokea eneo hilo mwaka 2011 na kusababisha kimbunga ambapo watu zaidi ya 18,000 walifariki.
Tetemeko hilo, moja ya mitetemeko mikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa, liliharibu kinu cha nyuklia cha Fukushima. Hadi sasa, shughuli kubwa ya kuondoa taka za nyuklia imekuwa ikiendelea.
Maafisa wa serikali wanasema hakujakuwa na dalili zozote za uharibifu kwenye kinu hicho wakati huu.
Maafisa wa Jiolojia wa Marekani awali walikuwa wamekadiria nguvu ya tetemeko hilo kuwa 7.3 lakini baadaye wakapunguza hadi 6.9, kipimo ambacho ni cha chini kuliko kile kilichotolewa na wenzao wa Japan.
Idara ya utabiri wa hali ya hewa ya Japan inasema tetemeko la sasa linauhusiano na tetemeko la mwaka 2011.
Msemaji mmoja aliyenukuliwa na Japan Times amesema eneo hilo limekuwa likipokea tetemeko la 7.0 angalau mara moja kila mwaka.
Kina cha tetemeko la Jumanne kinakadiriwa kuwa kilomita 30 chini ya ardhi (maili 18.6), JMA imesema.
Mitetemeko mikubwa imesikika maeneo ya mbali yakiwemo mji mkuu New York ulio maili 100 kusini mwa Fukushima.
Nyumba katika mji huo zilitikisika kwa karibu sekunde 30.
Japan huwa eneo linaloathiriwa sana na mitetemeko ya ardhi ambapo asilimia 20 ya mitetemeko ya ardhi ya nguvu ya 6.0 kwenda juu duniani hutokea eneo hilo.
Watu zaidi ya 50 walifariki kwenye mitetemeko miwili eneo la Kumamoto Aprili.
No comments:
Post a Comment