AUDIO: Askari polisi 6 wa Kikosi cha Usalama Barabarani Watumbuliwa Kwa Utovu wa Nidhamu
Askari polisi sita wa Kikosi cha Usalama Barabarani, wameondolewa baada ya kukiuka taratibu za kazi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Kamishana Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
ambaye pia ni Mkuu wa Operesheni, Kitengo cha Usalama Barabarani
Tanzania, Fortunatus Musilimu, alisema askari hao watapangiwa kazi
nyingine.
Kwa
mujibu wa Kamishna Musilimu, askari hao kutoka katika mikoa mbalimbali
nchini, waliondolewa wakati wa ukaguzi wa utendaji wa kazi kwa askari wa
kikosi hicho.
“Ukaguzi
huo ulifanyika nchi nzima katika barabara kuu kufuatia mpango mkakati
wa kupunguza ajali za barabarani nchini,” alisema kiongozi huyo wa
polisi.
Aliwataja
askari hao kuwa ni D 9363 Sajenti Richard aliyekuwa wilayani Misungwi,
Mkoa wa Mwanza, G 9958 PC, Edward, aliyekuwa eneo la Lilambo mkoani
Ruvuma, H 8234 PC Mungwe, aliyekuwa eneo la Tanesco Jimboni, wilayani
Mbinga, Mkoa wa Ruvuma na WP 3058 Koplo Mariam, aliyekuwa eneo la
Igurusi, Mbeya.
“Askari
hao walikutwa wakiwa hawakuvaa namba za Jeshi la Polisi kama
utambulisho wao kazini, kitendo ambacho ni utovu wa nidhamu na
kutozingatia maadili ya kijeshi.
“Yaani
kitendo cha kutovaa namba kiliashiria askari hao walikuwa wababaishaji,
walikuwa wakificha maovu, hawakuwa wawazi katika utendaji kazi wao na
pia waliashiria kujihusisha na vitendo vya rushwa.
“Mbali
na hao, askari wengine waliochukuliwa hatua ni D 9603, Sajenti Samwel
na G 8264, PC Dickson, waliokutwa eneo la Hanihani, wilayani Igunga,
Mkoa wa Tabora.
“Hawa
walikutwa katika mazingira yanayoonyesha walikuwa wakijihusisha na
vitendo vya waziwazi vya kudai rushwa kutoka kwa wenye magari
yaliyokuwa na makosa,” alisema Kamishna Musilimu.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani kufanya kazi kwa uadilifu ili wasichukuliwe hatua.
==>Msikilize hapa Kamanda Muslimu akifafanua sababu za uamuzi huo:-
No comments:
Post a Comment